Habari za Punde

*WANAFUNZI WATAKIWA KUACHANA NA TABIA ZA UTORO NA USHINDANI WA MAVAZI MASHULENI

MAMA SALMA AENDELEA NA ZIARA LINDI MJINI.Mke wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Mama Salma Kikwete akipokea zawadi ya kuku kutoka kwa wananchi wa Kata ya Makonde iliyoko katika Manispaa ya Lindi wakati alipofanya ziara ya kikazi katika kata hiyo, jana.

Wananchi wa Kata ya Makonde wakicheza ngoma ijulikanayo kwa jina la deda inayochezwa na watu wa kabila la Wamwela wanaoishi katika wilaya ya Lindi Mjini wakati Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mama Salma Kikwete alipotembelea tawini hapo jana. Picha na John Lukuwi

****************************************
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Wanafunzi wametakiwa  kuachana na tabia zisizoendana na maadili ya kiuanafunzi ikiwemo  utoro na mashindano ya mavazi bali wasome kwa bidii na kutengeneza mazingira ya kujisomea ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao kwani elimu inaweza kuwatoa katika hali duni ya maisha na  kuwaweka katika hali nzuri.
Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa akiongea  kwa nyakati tofauti na  wananchi wa kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro zilizopo katika  wilaya ya Lindi mjini wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kutoka wilaya hiyo.
Mama Kikwete ambaye pia ni MNEC alisema kuwa licha ya kuwa na tatizo la upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia lakini wanafunzi wengi wa siku hizi ni watoro, hawapendi kusoma, hawawatii wazazi na walimu wao, siyo wasikivu wawapo darasani  jambo linalosababisha kutofanya vizuri katika mitihani yao.
“Wanafunzi lazima mtambue kuwa elimu haina mwisho na elimu ndiyo msingi wa maendeleo, someni acheni tabia ya utoro na mkimaliza darasa la saba jiungeni na elimu ya sekondari, baada ya hapo msome hadi chuo  kikuu hali hii itasaidia  kupata wataalamu wengi zaidi na hivyo kupunguza tatizo la watumishi”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa wazazi aliwataka kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao na kuhakikisha kuwa wanakwenda shule na kuhudhuria madarasani na kutowaachia jukumu hilo walimu peke yao kwani kama watoto wao hawatasoma ni vigumu kwa mkoa huo kusonga mbele kimaendeleo kwa kuwa maendeleo hayapatikani bila ya kuwa na elimu.
“Maendeleo ya elimu katika mkoa wa Lindi ni mabaya ukilinganisha na mikoa mingine tatizo hili likiachwa kwa muda wa miaka 10 hali itakuwa mbaya zaidi. Suala la ufaulu mdogo wa wanafunzi lisiwakatishe tamaa na kuwarudisha nyuma bali nyote kwa pamoja wanafunzi, walimu, wazazi na viongozi wa Vyama vya siasa na Serikali mchukue hatua za makusudi ili muweze kuinusuru hali hii”, alisema Mama Kikwete.
Tatizo la utoro lilijidhihirisha pale ambapo zaidi ya wananafunzi 33 kutoka shule ya msingi Tulieni na juzi wanafunzi zaidi ya 40 wa shule ya msingi Kikwetu walihudhuria  katika mikutano ya hadhara  muda wa masomo  wakiwa pamoja na wazazi au ndugu zao na Mama Kikwete alipowauliza kwanini hawakwenda shule hawakutoa sababu za msingi.
Aidha Mama Kikwete pia aliwasihi  wananchi hao  kulima  mashamba yao, kupanda , kupalilia na kuvuna kwa ushirikiano kama walivyokuwa wakifanya miaka ya nyuma  na kuachana  na tabia ya  kila mtu kulima shamba lake peke yake kwani kwa  kulima kwa  ushirika kwa muda mfupi wanalima  hekari nyingi tofauti na kulima mtu mmoja mmoja.
Pia aliwataka  viongozi wa vyama vya Siasa na Serikali kuacha tabia ya kuchanganya lugha ya Kiswahili na kiingereza wakati wanajibu maswali au kuongea na wananchi kwa kuwa  wananchi wengi hawafahamu lugha hiyo zaidi ya lugha ya Kiswahili na hivyo kuwafanya wasielewe mambo mbalimbali ya maendeleo yao.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Jamuhuri Nelson Bebo alisema kuwa wakazi wa kata hiyo wamenufaika  na miradi ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe, ufugaji wa kuku wa kienyeji na mayai na ufugaji wa mbuzi na kujipatia kipato cha ziada ambacho kimeongeza pato la familia.
Akiwa katika kata za Jamhuri, Makonde na Ndoro Mjumbe huyo wa NEC alikabidhi  kadi  kwa wanachama  wapya wa CCM  47, Umoja wa vijana 32, Umoja wa Wanawake  52 na Jumuia ya Wazazi  39.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.