Habari za Punde

*YANGA YABANWA KOO NA POLISI MORO KWA SULUHU 0-0, SIMBA YANG'ANG'ANIWA NA TOTO 2-2, JULIO APEWA KICHAPO NA MCHEZAJI WA TOTO

 TIMU ya Yanga ya Dar es Salaam, leo imebanwa koo na Polisi Moro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, ambapo hadi mwisho wa mchezo huo timu hizo zimetoka suluhu 0-0 na kugawana pointi, ambapo sasa Yanga imefikisha jumla ya Pointi 49, huku Polisi Moro wakifikisha Pointi 18.
TIMU ya Simba nayo leo imeng'ang'aniwa na Toto Afrika katik mchezo wao uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba Jijini Mwanza. Katika mchezo huo timu hizo zimetoka sare kwa kufungama mabao 2-2.

KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo Julio, leo ameonja joto ya jiwe kwa kuonja mkong'oto kutoka kwa mchezaji wa Toto Afrika, ambaye alielezwa kuwa alikuwa amevalia Jezi No 5.
Sababu za Kocha huyo kupewa kipondo zimeelezwa kuwa ni kutokana na mchezaji huyo kuonekana akiiba mpira wa Simba na kuondoka nao mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ambapo pia mchezaji huyo alionekana na mashabiki waliokuwa jukwaani.

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Redio One, Julio alisema kuwa alipigiwa simu na mmoja kati ya mashabiki wa Simba aliyekuwa Jukwaani baada ya kumuona mchezaji huyo alibeba mpira huo na kuondoka nao, ambapo alimwambia kuwa mpira umechukuliwa na mchezaji aliyevalia jezi namba 5.

Baada ya Julio kupata taarifa hiyo aliamua kumfuata mchezaji huyo na kumueleza akiwa pamoja na walimu wake ambao walianza kumtetea, na ndipo mchezaji huyo alianza kumshambulia kwa kumchapa ngumi ya uso iliyomsababishia kuvimba jicho.

''Ama kwa hakika nasema hivi hewani nikijua kwamba nazungumza na vyombo vya habari, alichonifanyia mchezaji huyu, nitakuja kumfanyia kitu kibaya zaidi na hataamini macho yake, na wala siogopi kutoa vitisho hivi, kwani ameonyesha nidhamu mbaya tena mbele ya walimu wake, ukumbuke mimi ni Kocha wa timu ya Taifa nina haki ya kuwafundisha nidhamu wachezaji na hasa hawa ambao hawajabahatika kuja katika timu ya Taifa ili wasije kutupa aibu mbele ya safari, nasema nitalipiza na mtasikia''. alisema Julio

KATIKA matokeo mengine ya michezo ya Ligi kuu ya Vodacom, iliyochezwa leo ni JKT Oljoro 2 JKT RUVU 0
KAGERA SUGAR 3 MTIBWA SUGAR 1
AFRICAN LYON 1 COASTAL UNION 0
AZAM FC 1 RUVU SHOOTING 0

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.