Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari leo, katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam.
Nape amekanusha madai ya Chadema kwamba Kampuni ya Jitegemee inayomilikiwa na CCM imeshaIingia mkataba na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa Bandari Kavu, kwenye eneo lililokuwa na SUKITA jijini Dar es Salaam. Amesema, TPA ni miongoni mwa kampuni kadhaa ambazo zinaomba kulipata eneo hilo, lakini hakuna kampuni ilivyokwisharidhiwa hadi sasa. Picha na Bashir Nkoromo
**************************
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jana Aprili 3, 2013,
mmoja wa Viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema alitoa tuhuma dhidi ya Chama Cha
Mapinduzi kuwa kupitia kampuni ya Chama ya Jitegemee Trading Company, CCM
imeingia mkataba na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kwenye mradi wa upanuzi wa
Bandari kavu kwa kutumia eneo la SUKITA lililopo maeneo ya makutano ya barabara
ya Kawawa na Mandela ambalo ni mali ya CCM.
Tuhuma hizi zimechapishwa leo na baadhi ya
vyombo vya habari na hasa TanzaniaDaima zikidai “Chadema wameibua unaoitwa
ufisadi wa Mwakyembe wa kuipa CCM zabuni ya kupanua bandari”.
Kiongozi huyo wa Chadema alikwenda mbali kwa
kuishutumu Wizara ya Uchukuzi na Waziri wake Dokta Harrison Mwakyembe kwa madai ya kukiuka taratibu na kutoa zabuni ya upanuzi wa
bandari ya Dar es salaam kwa CCM kinyume na taratibu za manunuzi jambo ambalo
ni uongo.
Ukweli ni kwamba Kampuni ya Jitegemee Trading
Company ni mali ya CCM, na pia ni kweli kuwa kiwanja kilichotajwa ni mali ya
CCM kilichokombolewa kutoka zilizokuwa mali za SUKITA ambayo pia ilikuwa
kampuni ya CCM.
Lakini TPA na Jitegemee mpaka sasa hawajaingia
mkataba wowote. Eneo hilo limeombwa na wawekezaji wengi wakiwemo TPA na masharti
waliyopewa waombaji wote ni kuleta mapendekezo ya mipango yao ya kibiashara
kabla ya kufikia uamuzi wa nani anawekeza kwa ubia na Jitegemee kwenye eneo
hilo.
Wanachokiita wenzetu wa Chadema kuwa ati ni
zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Jitegemee na Mamlaka ya Bandari ni barua ya
TPA kwenda Jitegemee wakiomba ridhaa ya kushirikiana kuliendeleza Eneo la
kampuni hiyo ya Jitegemee lenye ukubwa wa zaidi ya ekta 100, katika mfumo wa
ushirikiano yaani "Joint Venture" kupitia utaratibu wa PPP (Public,
Private Partnership) jambo ambalo ni la kawaida sana kwani linafuata utaratibu
na sheria zote husika.
Kama nilivyokwisha
kusema Chama Cha Mapinduzi kinamiliki Kampuni ya Jitegemee, na kwamba pamoja na
umiliki huo, kampuni hiyo imekuwa ikitekeleza shughuli za uwekezaji kwa muda
mrefu kwa kufuata taratibu zote na sheria za nchi kwa ujumla.
Tunatambua kuwa Chadema kwasasa wanapitia wakati mgumu sana
kisiasa kutokana na kuanza kuvuna walichopanda kwa muda mrefu katika siasa za
nchi yetu.
Lakini pia tunatambua tabia ya viongozi wa Chama
hicho ya kudandia kila gari linalopita bila kujua linakokwenda kwa kugeuza kila
kinachofanyika nchini, ilimradi hakifanywi na wao basi ni haramu.
Hata hivyo mazingira haya wanayopitia hayawapi
uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kutofautisha barua ya
maombi ya kushirikiana kuendeleza eneo na mkataba!.
Aidha mazingira wanayopitia kwasasa hayawapi
uhalali wa kuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kushindwa kujua kuwa
kinachofanyika ni mawasiliano ya awali sana ya kusudio la kuendeleza eneo
husika na hakuna taratibu zilizokiukwa.
Umbumbumbu wa aina hii unatia mashaka sana juu
ya uwezo wao wa kufikiri na kupambanua mambo. Jambo moja wanaloonekana kulimudu
ni uwezo wao wa kutunga uongo na kupanga machafuko. Na hii ndio siri ya
watanzania kuwakataa kila kukicha na ndio siri ya kufa kwa chama hicho, kwani
njia ya muongo ni fupi.
Lakini tunazo taarifa kuwa uongo huu wamelishwa
na baadhi ya mafisadi waliotaka kutumia eneo hili la CCM kujaribu kukaa
katikati ya mwekezaji yeyote atakayejitokeza na Jitegemee kwa lengo la
kujinufaisha wao binafsi. Na huu ni mwendelezo wa Chadema kutumiwa na mafisadi
katika kutimiza mambo yao. Kutumika huku kunasukumwa na kiu yao ya kushika dola
kwa gharama yoyote. Watanzania tuwapuuze na kuwaepuka.
CCM inachukua nafasi hii
kuipongeza Wizara ya Uchukuzi kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya chini ya Dr.
Harrison Mwakyembe hasa ya kuongeza ufanisi kwenye bandari yetu ya Dar es
salaam. Tunawataka wasikatishwe tamaa na mafisadi wachache, wachape kazi kwa
uzalendo huohuo waliouonesha.
Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
ITIKADI NA UENEZI
04/04/2013
04/04/2013


No comments:
Post a Comment