Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo
akihutubia wanamichezo wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku mbili ya michezo
yaliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kulia ni mwezeshaji wa
mafunzo Dk. Tony Myers, wa kwanza kushoto ni Bi. Juliana Jones Yassoda ambaye
ni Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo na wa pili kushoto ni Mratibu wa mafunzo Dk.
Imani Silver Kyaruzi.
Mshiriki wa mafunzo ya michezo akikabidhiwa cheti cha kuhitimu mafunzo ya siku mbili na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Leonard Thadeo. Kutoka kulia ni Bw. Lihaya Henry Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo, Dk. Tony Myers ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo, wa kwanza kushoto ni Bi. Juliana Jones Yassoda Mkurugenzi Msaidizi wa Michezo na wa pili kushoto ni Mratibu wa mafunzo hayo Dk. Imani Silver Kyaruzi.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo kutoka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo wa tano kutoka kushoto,
akiwa katika picha ya pamoja na wakufunzi na washiriki wa mafunzo ya michezo ya
siku mbili yaliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Picha
na Benedict Liwenga
********************************************************
Na Genofeva Matemu – MAELEZO
WADAU wa Michezo wameshauriwa kuacha tabia ya kulalamika mara kwa mara pale wanaposhindwa katika mashindano ya michezo mbalimbali badala yake watumie mafunzo walioyapata ili kuendeleza sekta ya michezo Tanzania.
Ushauri huo ulitolewa jana jioni na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Bw. Leonard Thadeo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Fenella Mukangara wakati wa kufunga mafunzo ya michezo ya siku mbili yaliyoshirikisha wadau hao kutoka mikoa mbalimbali yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.
Alisema wamekuwa wakipata mafunzo hayo mara kwa mara, hivyo changamoto iliyoko kwao ni kwamba wanayatumiaje katika kuboresha sekta hiyo ili kuiwezesha Tanzania kushiriki na kushinda michezo ndani na nje ya nchi.
Aidha Bw. Thadeo amewataka wadau hao kuwa wabunifu na kujitahidi kutimiza wajibu wao kwa kutumia fursa waliyoipata kusaidiana na wanamichezo wengine waliowaacha mikoani ili kuweza kuboresha michezo kwa sababu wote goli lao ni moja la kutaka kuinua michezo Tanzania na kuweza kupata ushindi.
Aliwataka wadau hao kuwa wabunifu ili kubuni mbinu mbadala za kuinua sekta ya michezo Tanzania na kusaidiana na wanamichezo wengine waliopo mikoani.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatakuwa ni endelevu. Pia serikali ina mpango wa kuanzisha shahada ya pili ya michezo kwa njia ya mtandao ili kuinua michezo kuanzia ngazi ya chini hadi za juu.
Naye Mratibu wa mafunzo hayo Dk. Imani Silver Kyaruzi, aliwapongeza wadau hao kwa kuonyesha jitihada, kuchangia na kutaka kujifunza kuhusu masuala mbalimbali ya michezo.



No comments:
Post a Comment