Habari za Punde

*JITOKEZENI KUPIMA AFYA ZENU-DKT. NUNGU


Na Hussein Makame na Frank John-Maelezo
CHAMA cha Madaktari  Bingwa wa Upasuaji  Tanzania (TSA) kimewaomba wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na maeneo jirani  kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na upasuaji wa magonjwa mbalimbali.

Huduma hiyo itatolewa  bure kwa ushirikiano  kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na chama hicho, ambapo madaktari bingwa wa upasuaji wanatarajiwa kutoa huduma hizo kwa wananchi wa maeneo hayo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti  wa chama hicho, anayemaliza muda wake Dk.Kitungi Nungu wakati alipozungumza   na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo.  

Dk.   Nungu  alisema uchunguzi na upasuaji huo utatolewa  kwa magonjwa ya  mifupa, tumbo, matatizo ya njia ya haja ndogo na magonjwa ya kina mama katika  hospitali za mount Meru,Mbulu,Hydom,Machame na Babati.

Alisema  huduma hiyo,  itaanza kutolewa kuanzia  Aprili  11hadi 16  mwaka huu ambapo kila hospitali itakuwa na madaktari bingwa wasiopungua watano kwa ajili ya kutoa   matibabu  hayo  kwa  wakazi wa maeneo ya karibu na hosipitali hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti mtarajiwa wa chama hicho, Dk. Paul Marealle alisema huduma hiyo itafuatiwa na mkutano mkuu wa chama hicho na ule wa madaktari bingwa wa Afrika Mashariki,Kati  na Kusini mwa Afrika.

Aidha   Dk. Nungu  alifafanua kuwa mkutano huo utafanyika katika hoteli ya Snow-Crest iliyoko jijini Arusha  kuanzia  Aprili  17 hadi 19  mwaka huu, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kaulimbiu ya mkutano huo itakuwa ni ‘Ufundishaji wa Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Leo na Kesho’,. Katika mkutano huo  madaktari hao  watajadili jinsi ya kumpata  madaktari bingwa ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao nchini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.