Wachezaji wa Azam Fc, Erasto Nyoni (kushoto) Hamis Mcha (katikati) na Azizi Jabir, wakishangilia na kumpongeza Mcha baada ya kuifungia timu yake bao la tatu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Chamazi Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Azam imeshinda mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting. Na huko katika Kwingineko, timu ya Mbeya City, imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ashanti.
Kwa matokeo hayo sasa timu hizo za Azam Fc na Mbeya City, zimeishusha tena Yanga katika nafasi ya kwanza na ya pili na kurejea katika usukuni wa Ligi hiyo, huku Ynga ikirudi katika nafasi ya tatu, ikiwa na Pointi 25, huku Azam na Mbeya City zikiwa na Pointi sawa 26 kila moja, zikitofautina kwa magoli ya kufunga. Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry
Mabao ya Azam yalifungwa na Kipre Tchetche dakika ya kwanza ya mchezo huo kabla ya Joseph Kimwaga kushindilia msumari wa pili dakika ya 45 na Khamis Mcha akimalizia bao la mwisho dakika ya 70.
Mbeya City nao wamerudi katika nafasi yake ya pili baada ya kuinyuka Ashanti United kwa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Bao la kujifunga la Samir Ruhava dakika ya 38 liliisaidia Mbeya City kufikisha pointi 26 sawa na Azam FC lakini wakizidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mchezo mwingine uliochezwa leo, Mtibwa Sugar waliitumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kuifunga Rhino Rangers bao 1-0, bao lililofungwa na Salim Mbonde dakika ya 44.
Mshambuliaji wa Coastal Union, Uhuru Seleman (kushoto) akijiandaa kupiga shuti mbele ya beki wa Mgambo Shooting, wakati wa mchezo wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga leo jioni. Katika mchezo huo timu hizo zimetoka suluhu ya 0-0.
No comments:
Post a Comment