***************************************************
Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiendelea
na juhudi zake za kuimarisha Miundo
mbinu katika Sekta mbali mbali za Kiuchumi na Ustawi wa Jamii baadhi ya
Kampuni, Mashirika na hata wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi
wanaonekana kuzidi kushawishika na kasi ya
kutaka kuwekeza Zanzibar. KUSOMA ZAIDI BOFYA READ MORE
Shirika la
Kimataifa linaloshughulikia masuala ya usafirishaji wa anga la Transworld lenye
makamo makuu yake Dubai limefikia uamuzi wa kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya
mawasiliano ya anga kwa kujenga Kituo kikubwa cha uuzaji wa vifaa vya
ndege zinazopata hitilafu ya kiufundi ndani ya ukanda wa jangwa la
Sahara Barani Afrika.
Mwenyekiti
wa Shirika hilo Bwana Abdullah Al – Sulaimani alitoa kauli hiyo wakati Uongozi
wa Shirika lake ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi anayemaliza ziara yake
Dubai katika Muungano wa Mataifa ya Falme za Kiarabu { UAE }.
Bwana
Abdullah alimueleza Balozi Seif na Ujumbe wake kwamba Kituo hicho kitakachokuwa
na hadhi ya Kimataifa kinatarajiwa kutoa
huduma kwa ndege za aina ya boeing, Airbus, ATR pamoja na ndege zote
zinazotumia viwanja vya ndege vilivyomo ndani
ya Bara la Afrika.
Alieleza
kwamba awamu ya kwanza na huduma zitazotolewa
na kituo hicho zitalenga katika uuzwaji wa vifaa mbali mbali vya ndege
ambapo awamu ya pili itajikita zaidi katika kutoa fursa kwa ndege zenye kupata
hitilafu kupatiwa huduma za kiufundi kwenye kituo hicho.
Mwenyekiti
huyo wa Trasworld alifahamisha kwamba Mpango huo utakwenda sambamba na
utolewaji wa mafunzo kwa wananchi wazawa watakaopata nafasi ya kufanya kazi
kwenye Kituo hicho.
“ Kwa vile
sisi ni wazawa wa Visiwa vya Zanzibar hamu yetu ni kuona Elimu na fursa
tulizonazo huku tuliko pia tunazitumia kwa kuneemesha na nyumbani. Ahadi yetu
ya kutaka kuwekeza vitega uchumi nyumbani iko pale pale “. Alifafanua Bwana
Abdullah Al - Sulaimani.
Mwenyekiti
huyo wa Transworld alieleza kuwa Taasisi
yake pia iko tayari kutoa huduma bora na za kitaalamu kwa kutumia vifaa vya
kisasa katika upakuzi na upakizi wa mizigo kwenye uwanja wa ndege wa Zanzibar
endapo watapatiwa fursa hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kutokana
na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa ya sayansi na Teknolojia tabia ya
kuendelea kuchukuwa mizigo kwa kutumia mikono kwenye viwanja vya ndege imepitwa
na wakati.
“ Mambo ya
kuchukuwa mizigo kwa mikono haitakuwepo tena. Tunachotaka kuona Uwanja wa Ndege
wa Zanzibar unatoa huduma za usafiri wa anga katika kiwango kinachokubalika Kimataifa kabisa “. Alieleza Bwana Abdullah.
Akizungumzia
miradi mengine ya uwekezaji Mwenyekiti huyo wa Shirika la Kimataifa
linaloshughulikia masuala ya usafirishaji wa anga la Transworld alisema leseni
kwa ajili ya ufunguzi wa Benki ya Shirika hilo Zanzibar uko katika hatua za
mwisho.
Alisema
Benki hiyo itakuwa na uwezo wa kutoa huduma zaidi kwa Wananchi na hata wale
wawekezaji wanaoamuwa kutaka kuweka miradi yao ya kiuchumi na maendeleo Nchini
Tanzania.
“ Malengo
yetu ni kuhakikisha huduma zinazotolewa na benki hiyo hazilalamikiwi na wateja
kiasi ambacho mfumo wetu utaifanya iwe na hadhi ya pili katika kutoka huduma
ikitanguliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar Limited {PBZ } “. Alifahamisha Bwana
Abdullah.
Aidha
Mwenyekiti huyo wa Transworld alifafanua kwamba Taasisi yake iko katika hatua
za mwisho za kukamilisha taratibu zilizopo ili ijenge Hoteli kubwa nay a kisasa
Zanzibar itakayotowa huduma na kusaidia sekta ya Utalii Nchini.
Naye Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameuahidi Uongozi wa Shirika hilo la
Transworld kwamba Serikali ya Mapindujzi ya Zanzibar itahakikisha kwamba inatoa ushirikiano wa
karibu kwa shirika hilo ili kuona malengo yaliyokusidiwa kwa pande hizo mbili
yanatekelezwa kwa wakati.
Balozi Seif
alifahamisha kwamba masuala yote yatakayohitajika kutekelezwa kisheria likiwemo
suala la ardhi yanakamilishwa na Serikali kupitia taasisi zake katika kipindi
kifupi kijacho.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar aliviagiza vyombo na taasisi zinazohusika na masuala
hayo kuharakisha taratibu zinazohitajika ili kutoa fursa kwa wawekezaji hao
kuanza matayarisho kwa ajili ya miradi waliyoikusudia kuwekeza Zanzibar.
“
Nakuahidini kwamba yale masuala yote tuliyokubaliana na yanahitaji kufanyia
kazi kisheria likiwemo suala la ardhi wahusika nawaagiza kuyafanyia kazi na
utekelezaji wake ukamilike ndani ya wiki moja “. Alifafanua Balozi Seif.
Mazungumzo
hayo pia yalijumuisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Mh.
Nassor Ahmed Mazrui pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Othman Masoud
Othman.
Wengine ni
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,
makazi, Maji, Nishati na Madini Nd. Ali Khalil Mirza, Naibu Katibu Mkuu Wizara
ya Elimu Nd. Abdulla Mzee Abdulla na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji
Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } {Salum Khamis.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na ujumbe wake anatarajiwa
kurejea nyumbani Zanzibar kesho Jumanne Tarere 19 Novemba 2013 mnamo majira ya
saa 10.00 za jioni baada ya kumaliza ziara yake Nchini Marekani na Dubai.
Othman
Khamis Ame
Ofisi ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
18/11/2013.


No comments:
Post a Comment