MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amepinga agizo la Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, lililomtaka kuitisha Mkutano Mkuu wa Wanachama ndani ya siku 14,kwa lengo la kujadili malumbano yanayoendelea ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo mchana, Rage alisema kuwa, amesikitishwa sana na tamko lililotolea na TFF, lililomtaka aitishe mkutano mkuu badala ya kuanza kukemea vitendo vya kufanya mapinduzi visivyo fuata taratibu na kanuni za katiba husika.
“Kamwe siwezi kuvunja Katiba yangu kwa maelekezo ya TFF na siwezi kuitisha mkutano kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kupokonywa madaraka na majukumu yangu, tena mbaya zaidi napangiwa hadi ajenda ya kuzungumza na endapo TFF,watanilazimisha kufanya hivyo nitajiuzulu,’. alisema Rage.
Aidha Rage, alisema kwenye katiba ya Simba ibara ya 28 kifungu cha kwanza (a),(b),(c) na (d) kinamtambua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe saba siyo Kaimu Mwenyekiti ambaye hatambuliwi na Katiba hiyo wala ile ya TFF.
Na pia Katiba ya Simba ibara ya (22) inasema Makamu Mwenyekiti wa Simba anatambuliwa kihalali kwa kuchaguliwa na kupata kura 50 +1 na mwenye mamlaka ya kuitisha Kamati ya Utendaji ni Mwenyekiti na siyo mtu mwengine.
“Kwa mujibu wa vifungu hivyo Joseph Itang’are bado hajawa na uwezo wa kuitisha mkutano wa Kamati ya Utendaji kwa vile hatambuliwi na Katiba ya Simba,”alisema Rage.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na makosa yaliyofanywa na viongozi hao kwenye katiba ya TFF, Ibara ya 73 adhabu za viongozi hao ni kufungiwa kwa miaka 10 kutojihusisha na maswala ya soka kwenye klabu husika.
Katika mkutano huo Rage ameongelea mambo mengi ikiwemo tuhuma za kula pesa za usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi pamoja na fedha za udhamini wa Televisheni za ZUKU TV.
Pia kiongozi huyo alitumia mamlaka yake kama Mwenyekiti wa klabu ya Simba kumtangaza Michael Richard Wambura, aliyemteuwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji huku aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Rahma Al Kharoos, akiteuliwa kuwa Mdhamini wa klabu hiyo na kutangaza rasmi kufuta mkutano wa Tarehe moja.
Mapema wiki iliyopita Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo ilitangaza kumwengua Rage kwenye nafasi yake ya Uwenyekiti na nafasi yake kukaimiwa na Joseph Itang’are, na kuitaarifu TFF,ambayo nayo ilipinga mapindizu hayo na kumpa siku 14 kiongozi huyo kuitisha mkutano ili kumaliza mtafaruky huo ndani ya timu.

No comments:
Post a Comment