Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephrahim Kwesigabo, akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam kuhusu Siku ya Takwimu Afrika itakayo adhimishwa Dar es Salaam kesho.
Mkurugenzi wa Sensa ya
Watu na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephrahim Kwesigabo,
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu Siku ya Takwimu
Afrika itakayo adhimishwa Dar es Salaam kesho. Kulia ni Mtakwimu Mkuu, Adella
Ndesengia. PICHA NA VERONICA
KAZIMOTO – MAELEZO
*******************************
Na Veronica Kazimoto - MAELEZO
Tanzania itaungana na
nchi nyingine barani Afrika katika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika ambayo
itafanyika tarehe 27 Novemba, 2014 katika ukumbi wa mikutano uliopo Jumba la
Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo na
waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim
Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema lengo la kuadhimisha siku hiyo
ni kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa tasnia ya takwimu katika kuleta
maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani
Afrika.
Kwesigabo amesema kuwa,
Kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka 2014 ni “Takwimu Huria kwa Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa Wadau wote”.
“Kaulimbiu ya Siku ya
Takwimu Afrika kwa mwaka huu imebeba ujumbe muafaka ambapo kwa kuwa sasa
maendeleo ya Afrika yanategemea takwimu huria katika kuongeza uwajibikaji na
ushirikishwaji katika kuandaa sera, kupanga na kutathmini mipango mbalimbali ya
maendeleo na kufanya maamuzi sahihi, amefafanua Kwesigabo”.
Takwimu huria ni takwimu na taarifa
zinazozalishwa kwa ubora na viwango kutokana na tafiti au taarifa za kiutawala
ambazo zinatolewa, kusambazwa na kutumiwa na mtu yeyote bila kikwazo chochote.
Akielezea baadhi ya sifa za takwimu
huria Mkurugenzi Kwesigabo amesema ni pamoja na upatikanaji wake kwa urahisi
kulingana na mahitaji ya watumiaji, ziwe kamilifu kwa kutoa ujumbe sahihi na
unaoeleweka na ziwe katika mfumo
utakaomrahisishia mtumiaji kuzitumia
kulingana na mahitaji yake pasipo kizuizi chochote.
Sifa nyingine za takwimu huria ni
kutokuwa na ubaguzi, zitolewe kwa wakati, na muundo wa uhifadhi wake uwe rahisi
ambao unaweza kusomeka katika programu mbalimbali za kompyuta.
Kwesigabo
ameongeza kuwa Serikali ya nchi yoyote inapokuwa na
mfumo wa takwimu huria, huwezesha wananchi na wadau wengine kupata taarifa na
takwimu zinazozalishwa katika nchi hiyo bila kizuizi chochote. Aidha, huongeza
uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.
Washiriki mbalimbaliwa kutoka
katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Vyuo vya Elimu
ya Juu, Wanafunzi wa Shule za Sekondari pamoja na Wadau wengine wa takwimu
nchini wanatarajia kuhudhuria katika maadhimisho hayo.
Maadhimisho
ya Siku ya Takwimu Afrika hufanyika tarehe 18 Novemba, kila mwaka lakini kwa Tanzania
maadhimisho hayo yatafanyika kesho tarehe 27 Novemba, 2014.
No comments:
Post a Comment