Habari za Punde

*PLUIJM NUSURA AMCHAPE MAKOFI DIDA BAADA YA MCHEZO WA JANA, TWITE AWAKA KUIKACHA KAMBI

Kocha Mkuu wa timu ya Yanga Hans Van Der Pluijm, (pichani kulia) akimwakia kipa wake Deogratius Munish 'Dida' baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati yao na Stand United uliochezwa jana jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo Yanga ilishinda mabao 3-2, huku mabao hayo aliyofungwa kipa huyo yakionekana kuwa ni ya kizembe.
**************************************************
KUELEKEA kambi ya timu ya Yanga ya kujiwinda na michezo kadhaa ya Ligi Kuu Bara iliyosalia na ule wa Kimataifa kati yao na Etoile Du Sahel, ya Tunisia, Kocha wa timu hiyo Hans Van Der Pluijm, alitibuana na wachezaji wake baada tu ya kumalizika kwa mchezo kati yao na Stand United uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo Pluijm, alimfuata kipa wake Dida na kuanza kumfokea wakati wachezaji wakitoka uwanjani, huku akionesha kumlaumu kutokana na kufungwa magoli ya kizembe na kuifanya timu yake kuibuka na ushindi wa mbinde wa mabao 3-2.

Kocha huyo alipomalizana na Dida, alianza kumkoromea beki wake kiraka mwenye uwezo wa kucheza nafasi kadhaa uwanjani, Mbuyu Twite, ambaye kwa hakika katika mchezo wa jana alionekana kuziba viraka vingi kwa kucheza jihadi na kumdhiti vilivyo mshambuliaji wa Stand United, Mnigeria, Chidiebere.

Pluijm alisikika akimwakia Twite wakiwa wanaelekea vymba vya kubadilishia nguo, huku Twite naye akimjibu kwa sauti kupinga kile alichokuwa akiambiwa na kocha wake kuwa 'eti' alicheza chini ya kiwango na kusababisha magoli ya kizembe yaliyoiwezesha timu yake kufungwa mabao 2 kwa 3.

''Mi ntaondoka kambini na sikai kambini, siwezi kuvumilia kusemwa kama mtoto mdogo, wakati makosa yamefanywa na mtu mwingine uwanjani''. alisikika Twite akiwaka kwa sauti kumjibu kocha wake wakati wakielekea vyumbani.

Baada ya mchezo wa jana kocha huyo alionekana kuwa na hasira zaidi huku akiwawakia wachezaji hao Dida kwa wakati wake na Twite, ambapo alipozungumza na wanahabari baada ya mechi hiyo, alikiri kuwa timu yake haikucheza katika kiwango kilichotarajiwa na kudai kuwa hata ushindi huo wa jana waliupata kibahati tu. 

Yanga imebakiza michezo minne ili kukamilisha mzunguko wa Ligi hiyo, huku wakihitaji pointi 6 tu ili kutangaza ushindi, ambapo iwapo watafanikiwa kushinda katika michezo miwili ijayo basi watakuwa wamejikakikishia kutwaa taji hilo.

Mechi za Yanga zilizosalia ni Azam Fc, Ndanda Fc, JKT Ruvu na Polisi Morogoro.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.