Na Ripota wa Sufianimafoto, Shinyanga
MSHAMBULIAJI wa Yanga raia wa Zimbabwe Donald Ngoma, akicheza kwa juhudi kubwa na kujituma ameweza kuifungia mabao 2 timu yake katika dakika ya 8 na 75, huku mchezaji wa Mwadui aliyetokea benchi Bakari Kigodeko, akiingia kutibua shangwe za ushindi huo kwa bao la kusawazisha katika dakika ya 87 kwenye mchezo huo uliochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Sare hiyo hiyo sasa ni ya pili kwa timu ya Yanga kwa msimu huu, ambayo inawafanya mabingwa hao watetezi wafikishe jumla ya pointi 20, baada ya kucheza mechi nane, huku wakiendelea kubaki kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwa tofauti ya pointi moja tu dhidi ya wapinzani wao katika mbio hizo, Azam FC, ambao nao kesho wanashuka dimbani kucheza na JKT Uwanja wa Karume.
Mabao ya Donald Ngoma, alifunga akimalizia pasi nzuri ya Kiungo Andrey Coutinho katika kipindi cha kwanza na la pili akimalizia pasi ya deusi Kaseke katika kipindi cha pili.
Mwadui walisawazisha bao la kwanza katika dakika ya 40 kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Mbeya City, Paul Nonga kwa shuti kali baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga wakidhani ameotea.
Bao la pili la kusawazisha na Mwadui lilifungwa na Bakari Kigodeko, katika dakika ya 87, akimalizia mpira wa Athuman Iddi Chuji, aliyeingia kipindi cha pili.
Kikosi cha Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Andrey Coutinho, Thabani Kamusoko, Malimi Busungu, Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
Mwadui FC: Shaaban kado, Shaaban Hassan, Malika Ndeule, David Luhende, Emmanuel Simwanda, Joram Mgeveke, Anthony Matogolo, Jamal Mnyate, Jabir Aziz, Paul Nonga na Rashid Mandawa.
MATOKEO YA MECHI NYINGINE ZA LEO:-
YANGA SC 2 - MWADUI FC 2
NDANDA FC 0 - STAND UNITED 0
MTIBWA SUGAR 1 - KAGERA SUGAR 0
MBEYA CITY 1- MAJIMAJI 1
TOTO AFRICAN 1 - MGAMBO JKT 0
SIMBA SC 1 - COASTAL UNION 0
No comments:
Post a Comment