Mgeni rasmi ambaye pia
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akiongea na
wahitimu wakati wa mahafali ya 37 ya Bodi ya Taifa na Wakaguzi wa Hesabu nchini
(NBAA) na wageni waalikwa yaliyofanyika jana katika kituo cha NBAA Mbweni
jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahitimu wa Bodi NBAA wakifuatilia kwa
makini hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa mahafali ya 37 yaliyofanyika katika
kituo cha NBAA Mbweni jana jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya wahitimu 972
walipata CPA na wahitimu 87 walipata cheti cha utunzaji wa hesabu.
Mgeni rasmi ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akimpongeza mmoja wa wahitimu wa
CPA aliyefanya vizuri kwenye mitihani yake wakati wa mahafali ya 37
yaliyofanyika katika kituo cha NBAA Mbweni jana jijini Dar es Salaam.
Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyemaliza muda wake Ludovick Utto akimpa
mkono wa pongezi Mrithi wake katika nafasi hiyo Prof. Mussa Juma Assad wakati
wa mahafali ya 37 yaliyofanyika katika kituo cha NBAA Mbweni jana jijini Dar es
Salaam alipokwenda kupongezwa kwa taasisi yake kuendelea kuwatambua,
kuwapongeza na kutoa zawadi kwa wahitimu wanaofanya vizuri kwenye masomo yao ya
CPA.
Baadhi ya wahitimu wakijiaandaa kabla ya kuanza maandamano kuelekea eneo la kutunuku vyeti wakati wa mahafali ya 37 yaliyofanyika katika kituo cha NBAA Mbweni jana jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi ambaye pia
ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Bodi ya Taifa na Wakaguzi wa
Hesabu nchini (NBAA) na wahitimu CPA wakati wa mahafali ya 37 yaliyofanyika
jana katika kituo cha NBAA Mbweni jijini Dar es Salaam. Picha Eleuteri
Mangi-MAELEZO
************************************
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
Wahitimu wa Bodi ya
Taifa na Wakaguzi wa Hesabu nchini (NBAA) ambao ni wataalamu wa masuala ya uhasibu na
ukaguzi wa hesabu wameaswa kulinda, kutunza na kusimamia viapo vyao wakati
wakitekeleza majukumu yao ya kihasibu ipasavyo katika sehemu zao za kazi
Hayo yamesemwa na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Mark Mwandosya wakati wa mahafali ya
37 ya Bodi ya NBAA yaliyofanyika jana katika kituo cha NBAA Mbweni jijini Dar
es Salaam.
“Kiapo mlichoapa leo
kiwe chachu ya ufanisi katika utendaji wenu wa kazi, kushuka kwa kiwango cha
maadili katika utumishi kunatokana na kuota kwa mizizi katika suala la fedha”
Prof. Mwandosya aliendelea
kusisitiza, “Mlinzi mkuu wa fedha katika sehemu yeyote ile ni Mhasibu, nanyi
leo mnahitimu, mnapaswa kuwa waaminifu kwa familia zenu, taaluma yenu na kwa taifa mkiongozwa na kiapo mlichoapa,
isiwe ni sehemu ya ajenda ya leo ya kutimiza wajibu, bali kiapo hicho kiwe cha
kusisitiza maadili, uaminifu, uadilifu na uzalendo”.
Aidha, Prof. Mwandosya
aliongeza kuwa Bodi ya NBAA na Watanzania wana wajibu wa kujenga fikra ya
kizalendo kwa taifa lao na kujiamini katika masuala ya hesabu za fedha ili
waweze kufikia viwango vya kimataifa kwa kuweka misingi imara kwa wahasibu na
wakaguzi wa hesabu ambapo mataifa mengine wavutiwe kuja kujifunza hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Mtendaji Bodi ya Taifa na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) Bw. Pius Maneno
akitoa taarifa ya Bodi hiyo kwa mgeni rasmi wakati wa maafali hayo alisema kuwa
kituo hicho kimefanikiwa kinatoa mchango mkubwa nchi katika kukuza fani ya
wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya
nyuma.
Katika mahafali hayo,
idadi ya wahitimu imeongezeka mwaka huu na kufikia 972 waliopata CPA na wahitimu
87 kwa ngazi ya cheti cha utunzaji wa hesabu tofauti na hali ilivyokuwa mwaka
jana 2014 ambapo kulikuwa na jumla ya wahitimu 855 walipata CPA na wahitimu 82
walipata cheti cha utunzaji wa hesabu.
Wakati huo huo, mmoja
wa wahitimu hao Imelda Mzatulla alisema kuwa kiapo walichoapa kinawahamasisha
kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa kanuni za maadili ya kiuhasibu na ukaguzi wa
hesabu, kwa uaminifu, uadilifu na utaalamu kwa kuzingatia matarajio ya
Serikali, muajiri, jamii na taifa kwa ujumla.
Kiapo hicho walichoapa
wahitimu hao, pia kinawahimiza kuwa waendelee kushirikiana na kituo hicho cha
NBAA kwa kuzingatia miongozo yote ya taaluma yao inayotolewa na Bodi hiyo
nchini.
No comments:
Post a Comment