Na Beatrice Lyimo-Maelezo, Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la pili la kitaifa la wadau wa afya nchini linalotarajiwa kufanyika nchini kuanzia tarehe 11-13 Novemba mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ( Alhamisi Oktoba 8, 2015) Jijini Dar es salaam Rais wa Tanzania Health Summit Dkt. Omary Chillo alisema lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wadau wa afya kutoka sekta za umma na binafsi ili kujadili kwa pamoja namna bora ya kutatua changamoto na kuboresha huduma za afya nchini.
“Zaidi ya taasisi 100 za afya na wataalamu wa afya wapatao 1000 kutoka ndani na nje ya nchi wanataraijiwa kushiriki katika mkutano huu ukiambatana na mijadala muhimu inayohusu sekta ya afya, tafiti za kisayansi, kubadilishana ujuzi pamoja na maonyesho ya huduma, ubunifu na vifaa tiba” alisema Dkt. Chillo.
Aidha Dkt Chillo amefafanua kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma bora za afya hivyo ufumbuzi endelevu utapatikana kwa kukaa pamoja, kujadili na kupanga kwa pamoja ili kutatua kero na kuboresha huduma za afya.
Dkt. Chillo alisema kongamano hilo linaratibiwa kwa kushirikiana na Wizara ya afya na ustawi wa jamii, Tindwa Medical and Health Services, Association of Private Health Facilities in Tanzania, Christian Social Services Commision na Baraza Kuu la Waislam Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt. Chillo alisema zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma za afya nchini, ingawa zipo changamoto kadhaa ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja baina ya sekta ya umma na binafsi.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni “jinsi uwekezaji, ubunifu na falsafa ya mpango wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya afya vinavyoweza kuwa chachu ya mafanikio ya uboreshaji wa huduma za afya hapa nchini”.
No comments:
Post a Comment