Habari za Punde

*TOTO AFRICANS WAMUAGA KOCHA WAO KWA KIPIGO CHA MABAO 5-0 DHIDI YA AZAM FC

Na Ripota wa Sufianimafoto.com
TIMU ya Toto Africans leo imetoa mpya kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, baada ya kuingia uwanjani hapo wakiwa na bango lenye ujumbe wa kumuaga Kocha wao Mjerumani aliyeripotiwa kutangaza kuiaga timu hiyo baada ya mchezo wake wa leo na kurejea nchini kwao.
Nao Azam FC wakitumia mwanya huo leo wamefanikiwa kuwashusha tena wapinzani wao Yanga na kuerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Toto Africans Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kwa ushindi huosasa  Azam Fc wanafikisha jumla ya pointi 25 baada ya kucheza mechi tisa, ikiwazidi kwa pointi mbili, mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 23. 
Katika mchezo huo, ambao wachezaji wa Toto waliingia na bango la kumuaga rasmi kocha wao, Mjerumani Martin Grelis, Azam FC walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza 3-0.
Beki wa kulia Shomary Kapombe alifunga mabao mawili dakika za 34 na 36 mara zote akimalizia kazi nzuri ya winga Farid Mussa, na la tatu likifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 45 akimalizia pasi ya kisigino ya Didier Kavumbangu.

Na mabao hayo yalikuja baada ya Toto kumpoteza kipa wake wa kwanza, Mussa Mohammed aliyeumia dakika ya 18 na nafasi yake kuchukuliwa na kipa wa pili, Said Omar. 
Azam FC nayo ilipata pigo dakika ya 33 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Himid Mao kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Mnyarwanda, Jean Baptiste Mugiraneza.
Kipindi cha pili, Azam FC waliendelea kung’ara baada ya kupata mabao mawili, yaliyofungwa na Kavumbangu dakika ya 45 kwa shuti akimalizia pasi ya Ramadhani Singano ‘Messi’ na dakika ya 63 kwa shuti pia akimalizia pasi ya Mudathir Yahya.
Mchezo ulisimama kwa dakika zaidi ya 10 dakika ya 80 baada ya refa Anthony Kayombo kumruhusu kipa wa Azam FC Aishi Manula aende ‘kujisaidia’.

Mugiraneza pia alitoka dakika ya 70 kwenda maliwatoni, ingawa yeye hakuathiri mchezo kusimama.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, JKT Ruvu wamepata ushindi wao wa kwanza msimu huu, baada ya kuilaza 2-0 African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mabao ya Mussa Juma dakika ya 18 na Samuel Kamuntu dakika ya 90.
Kikosi cha Azam FC: Aishi Manula, Shomary Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Himid Mao/Jean Mugiraneza dk33, Ramadhani Singano, Frank Domayo, Farid Mussa/Mudathir Yahya dk56, Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche/Alan Wanga dk52. 
Toto Africans: Mussa Mohammed/Said Omar dk18, Erick Mlilo, Salum Chuku, Hamisi Suleiman, Hassan Khatib, Abdallah Seseme, Japhet Vedastus, Edward Christopher, Waziri Shentemba/Madinda Ramadhani dk59, Evarist Bernard na Miraji Athumani.

MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
Leo; Novemba 1, 2015
Prisons 2-2 Ndanda FC
African Sports 0-2 JKT Ruvu
Azam FC 5-0 Toto Africans
Jana; Oktoba 31, 2015
Simba SC 6-1 Majimaji FC
Kagera Sugar 0-2 Yanga SC
Mtibwa Sugar 4-1 Mwadui FC
Coastal Union 1-1 Mbeya City
Kesho; Novemba 2, 2015
Mgambo Shooting Vs Stand United

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.