JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
TAHADHARI KUHUSU KUINGILIA AU KUFUATILIA
MAWASILIANO YA WATU
Katika
siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kuwepo kwa Programu (Application)
ya simu ikijulikana kama SOFTBOX
TANZANIA iliyosemekana iko kwenye Google PLAYSTORE.
Ilidaiwa
kuwa program (Application) hiyo ya SOFTBOX
TANZANIA ilikuwa na uwezo wa kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe
mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi.
Kwa
yeyote aliyekuwa na nia hiyo ya kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe
mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu mwingine
alihitajika kulipia fedha kiasi cha Tshs 35,000/= kupitia mitandao ya simu ili
kupata namba ya siri kwa ajili ya kuwezesha nia hiyo.
Mamlaka
ya Mawasiliano imefanya uchunguzi kubaini kuwepo kwa programu hiyo na ukweli
kuhusu uwezo wake wa kufanya kilichodaiwa, ikiwa ni pamoja na kuangalia madhara
ya program hiyo na sheria inasema nini kuhusu suala hili. Baada ya kufanya
uchunguzi wa kina, Mamlaka ya Mawasiliano ilibaini na imejiridhisha kuwa
program (Application) hiyo haina uwezo huo wa kunasa au kuingilia
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka
kwenye simu ya mtu binafsi kama ilivyodaiwa.
Aidha
Mamlaka imebaini kuwa watengenezaji (Developers) wa programu hiyo
walikuwa na nia ya kutapeli na kujipatia fedha hiyo kiasi cha Tshs 35,000/= kwa
njia ya udanganyifu wakitumia kivutio cha kunasa au kuingilia mazungumzo ya
simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu za watu
binafsi.
Programu
(Application)
nyingine ya aina hiyo iliibuka tena ikiitwa SIMNET Tanzania ikiwa na maelezo kama ya awali.
Wakati
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania pamoja na Jeshi la Polisi wakiendelea na
uchunguzi zaidi, tunapenda kuuarifu umma wa Watanzania kuepuka kufanya mambo yafuatayo:
- Kuvutiwa na matendo yaliyo kinyume na sheria na maadili ya matumizi mazuri ya mawasiliano kama hili la kunasa au kuingilia mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi pamoja na mawasiliano ya WhatsApp kutoka kwenye simu ya mtu binafsi. Kitendo hiki ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 6 na 10 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na kifungu cha 123 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya Mwaka 2010. Sheria katika vifungu hivyo inakataza mtu yeyote kuingilia mawasiliano ya mtu mwingine. Adhabu kali ya makosa haya ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
- Mamlaka inawatahadharisha watumiaji wa huduma za mawasiliano kutokuwa wepesi na kudanganyika kufanya malipo yoyote kwa njia ya mitandao kwa huduma wasiyokuwa na uhakika nayo au bila kujiridhisha na uwepo wa huduma hiyo. Ni vizuri kutoa taarifa kwa mtoa huduma wako au kuwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano kupitia barua pepe malalamiko@tcra.go.tz au kupiga simu namba 0784558270/1.
Imetolewa
na:
Mkurugenzi
Mkuu
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania
04/12/2015
No comments:
Post a Comment