Na
Jacquiline Mrisho- MAELEZO
Serikali
kupitia Wizara ya Nishati na Madini imezindua mfumo wa malipo ya ada za leseni
za madini kwa njia ya mtandao ujulikanao kama Online Mining Cadastre
Transactional Portal (OMCTP).
Akiongea
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia
leseni Bw. John Nayopa amesema kuwa mfumo huu wa kielektroniki unawawezesha
wateja waliosajiliwa kutuma maombi ya leseni, kuhakiki taarifa za leseni wanazomiliki
pamoja na kutuma taarifa za utendaji kazi kwa njia ya kielektroniki.
“Wizara
ya Nishati na Madini imeanzisha mfumo huu kwa malengo ya kurahisisha
upatikanaji wa taarifa za leseni, kuongeza kasi za utoaji wa leseni za madini,
kupunguza tatizo la mlundikano wa maombi kwenye ofisi za madini na pia
kurahisisha mawasiliano kati ya Wizara na wamiliki wa leseni,” alisema Nayopa
Aidha,
Bw. Nayopa aliongeza kuwa mfumo huu wa kielektroniki unawawezesha wateja kupata
ramani za kijiolojia na takwimu mbalimbali za madini pia inamrahisishia mteja
kulipia ada za leseni kwa njia mbalimbali zikiwemo za mitandao ya simu, Maxmalipo,
kadi za Benki pamoja na kuhamisha fedha kupitia Benki.
Pia
Nayopa alizitaja nyaraka zinazohitajika ili kujisajili na mfumo huo wa
kielektroniki kuwa ni pamoja na fomu za kuomba usajili ambazo zinapatikana
kwenye tovuti za Wizara, leseni halisi pamoja na stakabadhi za malipo ya leseni
husika.
Aidha,
aliwataka wadau wengine ambao hawamiliki leseni wawasilishe fomu za usajili pamoja
na hati za utambulisho na kuwataka wamiliki wanaowatuma mawakala kuwapa nguvu
za uwakili (Power of Arttorney) ambazo zitawaruhusu mawakala hao kushughulikia
leseni.
Nayopa
amewataka wachimbaji wa madini nchini kujisajili kwenye ofisi za Madini ili
kuendelea kutumia huduma za leseni kwa njia ya mtandao kwakuwa malipo ya ada za
leseni yatafanyika kwa njia ya mtandao pekee.
Mpaka
sasa Wizara ya Nishati na Madini imefanikiwa kusajili jumla ya leseni 8800 za madini
nchini kwa kutumia mfumo huu wa kielektroniki ambapo idadi hiyo inajumuisha
leseni za Kampuni, vikundi na watu binafsi.

No comments:
Post a Comment