Habari za Punde

*WANANCHI WATAKIWA KULINDA AFYA ZAO KWA KUNUNUA DAWA KWENYE MADUKA YENYE WAFAMASIA WANAOTAMBULIKA KISHERIA

Na. Magreth Kinabo – MAELEZO, Dar es Salaam.
WANANCHI wameshauriwa kununua dawa za kutibu magonjwa mbalimbali wanazoandikiwa na madakatari  kwenye maduka ya dawa yenye Mfamasia mwenye elimu ya shahada ili kulinda  afya zao kwa kupata dawa sahihi.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es salaam na Msajili wa Baraza la Famasi Tanzania, Elizabeth  Shekalaghe  wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanyika kwa semina ya kutoa vyeti vya Usajili wa Wafamasia wapya iliyoambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo Nadhiri ya kiapo cha uaminifu kwa Wafamasia ambao walipewa kitabu cha miiko ya taaluma  yao.
Akizungumza wakati wa Semina hiyo Msajili huyo alipiga marufuku tabia ya baadhi ya wafamasia kutundika vyeti vya taaluma zao kwenye maduka ya dawa kwa lengo la kuonyesha uhalali wa kutoa huduma wakati wao wenyewe hawapo  katika famasia husika.

Aidha, Bi. Shekalaghe  alipiga marufuku  dawa zenye nembo ya Serikali kuuzwa kwenye maduka ya dawa yasiyomilikiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na kuongeza kuwa mfamasia  yeyote atakayekutwa na dawa zenye nembo Serikali katika duka analolisimamia, yeye pamoja na mmiliki watachukuliwa hatua za kisheria.

"Ni marufuku kwa dawa zenye nembo ya Serikali kuuzwa katika duka la dawa lisilomikiwa na Bohari Kuu ya Dawa(MSD).Mfamasia  ambaye duka analolisimamia litakutwa na dawa zenye nembo ye Serikali, yeye pamoja na mmiliki wake watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisisitiza Elizabeth.

Msajili huyo alisema  jamii inapaswa kuwatambua watu wanaotoa huduma za dawa, ambao wapo wenye elimu ya taaluma hiyo kuanzia ngazi ya Stashahada ambao huitwa Mafundi Dawa Sanifu na wale  wenye elimu ya Cheti cha mwaka  mmoja na wale wenye elimu ya program maalum wanaoitwa watoa dawa.

Alisisitiza kuwa jamii inapaswa kuwa na uelewa na kutofautisha kati ya duka la dawa,ambalo lazima liwe na Mfamasia na duka la dawa muhimu ambalo huwa  na watoa dawa. Aidha aliwataka wafamasia hao kukubali kwenda kufanya kazi mikoani ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata huduma stahiki za.

“ Kukutana kwetu  hapa kuna umuhimu  mkubwa ikizingatiwa kuwa sasa usimamizi wa utoaji wa huduma za dawa na majengo unalegalega,Tukiweza kuboresha utendaji wetu katika taaluma hii hususan usimamizi wa sehemu za kutolea huduma za dawa tutarudisha hadhi ya taaluma na kulinda afya ya jamii kwa kuwa na matumizi sahihi ya dawa,”alisisitiza Elizabeth.

Aliongeza kuwa Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko,kesi na migongano kati ya wafamasia na waajiri wao kutokana na kutoa huduma zisizokidhi viwango huku wengine wakifikishwa mahakamani kwa kutuhumiwa kuiba dawa.

“Yote  haya yanaonesha kwamba kuna tatizo na maadili na miiko ya kitaaluma kutofuatwa. Baraza la Famasi kama chombo cha Serikali haliwezi kubaki nyuma kama kisiwa katika kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.Ni vema tukakumbuka kwamba hivi sasa tunatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sera ya Serikali iliyoko madarakani kwa kauli mbiu ya HAPAKAZI TU,ambayo sisi sote tunapaswa kuielewa,kuitafsiri na kuisimamia katika namna ambayo itaonesha mabadiliko makubwa ambayo ndio lengo letu kama wataalum"

Aliwataka wafamasia hao kutii sheria bila shuruti na kuzisoma na kuzielewa sheria na kanuni zilizopo.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa baraza hilo Bw. Lagu Mhangwa aliwataka wafamasia hao kuwa na tabia kujiendeleza kielimu ili kuendana na mabadiliko ya taaluma ya dawa yanayotokea na kuandika miradi mbalimbali ambayo itakayowasaidia kubadilisha taaluma ya fani hiyo nchini.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.