Habari za Punde

*KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE KUKUTANA DAR ES SALAAM KUANZIA TAREHE 14 MACHI HADI 15 APRIL 2016

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGE LA TANZANIA  
Simu: +255 022 2112065-7 Fax No. +255 022 2112538 E-mail:  info@bunge.go.tz    
                     Ofisi ya Bunge,                  S.L.P. 9133,       DAR ES SALAAM
  
TAARIFA KWA UMMA  
KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE KUKUTANA DAR ES SALAAM  KUANZIA TAREHE 14 MACHI HADI 15 APRILI, 2016
 
1.0 UTANGULIZI kwa  kuzingatia matakwa ya Kanuni ya 117 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016, Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 14 Machi hadi tarehe 15 Aprili 2016 kutekeleza Majukumu yake, Jijini Dar es Salaam kabla ya Mkutano wa Bajeti wa Bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 19 Aprili, 2016. 

Hivyo, Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo jumapili tarehe 13 Machi 2016 tayari kwa kuanza vikao siku  ya tarehe 14 Machi, 2016. 

2.0       SHUGHULI ZITAKAZOTEKELEZWA Wakati wa vikao vya Kamati, Jukumu la Msingi katika Vikao hivyo kwa kamati zote litakuwa ni Majadiliano katika ngazi ya Kamati za Bunge na Serikali kuhusu maudhui ya Mpango wa Mwaka wa Maendeleo ya Taifa na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017. 

Aidha, ratiba ya Majukumu ya Kamati hizo yatatekelezwa kwa utaratibu  ufuatao: 
a) Kuanzia Tarehe 14 hadi 27 Machi, 2016 Kamati zitakuwa na Vikao kwa ajili ya kujadili Taarifa mbalimbali za Serikali ambapo kila Kamati itakutana na Viongozi na Watendaji wa Serikali kutoka katika Wizara au taasisi inayoisimamiwa na kamati husika.

b) Tarehe 29 Machi, 2016 Kamati zote za Bunge zitapokea Dondoo na Randama za Vitabu vya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

c) Siku ya Tarehe 30 Machi, 2016 Wabunge wote watapokea Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo ya Taifa na kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali  kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

d) Kuanzia Tarehe 31 Machi hadi Tarehe 06 April 2016 Kamati ya Bajeti itachambua mapendekezo ya mpango na kiwango cha Ukomo wa Bajeti. Wakati huo huo, 

e) Kamati za Kisekta zitafanya zitatembelea na kukagua utekelezaji miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016) na Wizara au Taasisi zinazozisimamia. 

f) Baada ya kutembelea miradi ya Maendeleo, kuanzia Tarehe 07 hadi 15 Aprili 2016, Kamati zitapokea na kuchambua taarifa za utekelezaji wa Bajeti za wizara zinazozisimamia kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kuchambua makadirio ya Matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata, 2016/2017

g) Kamati ya Fedha na Mtambuka zitaendelea na Shughuli za  uchambuzi juu ya masuala ya Fedha, UKIMWI, Bajeti na Sheria Ndogo. 

3.0  SHUGHULI NYINGINE Shughuli za Kamati zitamalizika tarehe 15 Aprili, 2016 Jijini Dar es Salaam ambapo Mkutano wa Bunge wa Bajeti utaanza tarehe 19 April, 2016 Mjini Dodoma na unategemewa kumalizika kabla ya  tarehe 30 Juni, 2016. 

Ratiba zote za Kamati zitapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz  
Imetolewa na: 

Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge Dar es Salaam 10 Machi,  2016.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.