Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na Kampuni ya TRUMARK katika ukumbi wa Kingsolomon Kinondoni jijini Dar es salaam jana March 05,2016.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiangalia Bidha katika maonesho ya Vikundi vya Wajasiriamali wa Vikoba kutoka katika taasisi mbalimbali kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Kampuni ya TRUMARK katika ukumbi wa Kingsolomon Kinondoni jijini Dar es salaam jana jioni March 05,2016. kulia Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Khamis Kigwangala.
**************************************
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imejizatiti katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo nchini.
Samia ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza katika tamasha la mwanamke lililofanyika jana usiku (Machi 5) katika ukumbi wa King Solomon, Jijini Dar es salaam.
Tamasha hilo liliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la True-Mark likibeba ujumbe wa "Pamoja Tunafanikisha" ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo yatafikia kilele chake Machi 8.
Mada kuu katika tamasha hilo ilikuwa ni kujadili lengo Namba 5 la Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu linalosisitiza kufikia usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana ifikapo mwaka 2030.
Makamu wa Rais alisema katika kufanikisha jitihada hizo serikali iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kupunguza changamoto zilizopo zikiwemo za unyanyasaji wa kijinsia ili kuharakisha upatikanaji wa uwiano sawa wa kijinsia.
Aidha, Samia alisema jitihada hizo za serikali za kuleta usawa wa kijinsia zinaweza zikapata mafanikio zaidi iwapo zitaungwa mkono na wanawake wenyewe kwa kuwa tayari kubadilika katika suala zima la malezi ya watoto na matendo yao kwa ujumla.
"Ni sisi wanawake wenyewe tumeleta tofauti hizi za kijinsia kupitia malezi; ni ukweli usiopingika kwamba watoto wote wanazaliwa sawa hakuna aliye bora zaidi ya mwingine. Lakini matendo yetu sisi wenyewe....huku mila, desturi zinatuletea tofauti hizi," alisema Samia na kuongeza
"Wanawake tubadilike katika malezi ya watoto wetu, tuwaone wote ni watoto, ingekuwa mmoja ni bora zaidi kuliko mwingine, Samia Suluhu asingekuwa hapa leo."
Samia alitumia fursa hiyo kuelezea jitihada za serikali za ukusanyaji wa mapato na kuhimiza wanawake kuunga mkono jitihada hizo kwa kufichua maovu ili serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha ambayo yataiwezesha kutoa huduma yenye uwiano sawa wa kinjisia.
Katika hatua nyingine aliwakumbusha wanawake kuongea na watoto wao kujikinga na maradhi ya ukimwi na kusema taarifa zilizopo maambukizi mapya ya ugonjwa huo yanawakumba zaidi vijana wa umri wa kati ya miaka 15-24.
Katika kongamano hilo Makamu wa Rais alipata nafasi ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ya bidhaa zinazotengenezwa na akina mama na kusikia mada mbalimbali zilizowasilishwa zikiwemo za masuala ya afya na uchumi.
Kauli mbiu ya jumla ya siku ya wanawake duniani mwaka huu ni "Ahadi ya Usawa" na kwa upande wa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa, kaulimbiu ni "50 kwa 50 Chukua Hatua ya Usawa" jambo ambalo Makamu wa Rais alisema Tanzania ilianza mapema ambapo suala la 50 kwa 50 limo ndani ya Katiba inayopendekezwa.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
06/03/2016
No comments:
Post a Comment