TIMU ya Simba leo imerejea tena kileleni mwa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara baada ya kuifunga Ndanda FC ya Mtwara kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Simba wamerejea kileleni baada ya kufikisha jumla ya Pointi 51 wakiwa mbele kwa pointi moja dhidi ya watani zao Yanga waliowaengua wekundu hao juzi waliporejea kileleni kwa kishindo walipowachabanga Wana Kimanumanu kwa mabao 5-0 nakufikisha jumla ya pointi 50.
Kwa ushindi wa leo umeipaisha tena Simba na kufikisha pointi 51 na mabao 40. huku Yanga wakiwa na Pointi 50 na mabao 51 wakati timu inayoshika nafasi ya tatu ni Azam FC wakiwa na 47, lakini wakiwa na mechi za vipolo na Simba wakiwa tayari wamecheza mechi 22 na Yanga wakiwa tayari wamecheza mechi 21.
Katika mchezo huo Simba walianza kupata bao la kwanza katika dakika ya 36 kupitia mchezaji wake Mwinyi Kazimoto,akiunganisha krosi ya Hassan Kessy na bao hilo kudumu hadi kumalizika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Mabao mengine ya Simba yalipatikana katika kipindi cha pili, mfungaji akiwa raia wa Uganda Hamisi Kiiza, aliyefunga baola pili katika dakika ya 57 kwa kichwa, akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Ibrahim Ajibu ambaye dakika 11 baadaye alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Danny Lyanga.
Bao la tatu kwa Simba lilifungwa katika dakika ya 72, baada ya Kiiza kuinasa pasi ya Lyanga na kuupachika mpira kimiani. Kabla ya mpira kumfikia Lyanga na kutoa pasi, kiungo Justice Majabvi aliachia shuti kali lililotemwa na kipa wa Ndanda na mpira kumfikia Lyanga.
Hata hivyo, ushindi huo haukuwa mwepesi kwa Simba, kwani Ndanda iliyokuwa na nyota kama Atupele Green, Kigi Makasi, Omega Seme, Salvatory Ntebe na wengine, licha ya kufungwa walionesha kandanda safi. Matokeo hayo yanaiacha Ndanda katika nafasi yake ya nane, ikiwa na pointi 24 ilizovuna katika michezo 21.
KIKOSI CHA SIMBA: Vicent Angban, Hassan ramadhani, Mohamed Hussein, Novaty Lufungo, Juuko Murshid, Justine Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonaes Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrahim Ajib na Said Ndemla.
KIKOSI CHA NDANDA FC: Jeremias Kisubi, Azizi Sibo, Paulo Ngalema, Kassian Ponela, Salvatory Ntebe, Hemed Khoja, William Lucian, Omega seme, Omary Mponda, Atupele Green na Kigi Makasi.

No comments:
Post a Comment