Habari za Punde

*WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWAPONGEZA WASANII WA FILAMU NCHINI

  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akipokea Tuzo kutoka kwa msanii wa Bongo Movie Elizabeth Michael (Lulu) wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam,leomchana .Anayeshuhudia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia James Wambura. Tuzo ya Africa Magic Viewers Choice ambapo amekuwa msanii bora wa Kike wa Afrika Mashariki kupitia filamu ya Mapenzi ya Mungu.
Na: Immaculate Makilika MAELEZO
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  amesema Serikali imefarijaka kwa ushindi wa wasanii wa filamu nchini walioshinda tuzo za  filamu Afrika za mwaka 2016(African Magic Viewers Choice Award) ziliyofanyika jijini Lagos nchini Nigeria mwishoni wa wiki iliyopita.

Waziri Mkuu Majaliwa, amesema hayo leo katika ukumbi wa mikutano ulipo katika  Ofisi yake  Jijini Dares Salaam, alipokutana na washindi wa tuzo za  filamu Afrika za mwaka 2016 (AMVCA)  ambao ni  Elizabeth Michael ‘Lulu’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Afrika Mashariki na Single  Mtambalike ‘Richie’ aliyeshinda tuzo ya Filamu Bora ya Kiswahili pamoja Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Mhe. Annastazia Wambura,Katibu Mkuu wa wizara Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi Joyce Fisso na wasanii wa filamu.

“Serikali imefarijika sana kwa nyie kwenda Nigeria na kushinda na mmetumia lugha ya Kiswahili, lazima tutumie nafasi hii kuwatangaza pia mmuendelee na fani hii ili kuvutia wengi zaidi” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza wasanii hao na kusema kuwa  Serikali itaendelea kushirikiana  na wasanii wakati wowote na amewataka kujipanga vizuri kutumia vyama vyao vya sanaa na kusisitiza kuwa  Mhe.  Rais John Pombe Magufuli ametoa matamko kadhaa  kuhusu sanaa  na wasanii  na ameendelea kushughulikia malalamiko yao ikiwemo suala la COSOTA, na kusema kuwa  baada ya taratibu zote kukamilika  suala hilo litasimamiwa na Wizara inayohusika na kazi za Sanaa.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia amewataka watanzania kuacha tabia ya kutojiamini  na kujidharau, na kuwataka watu waige mfano kwa wasanii hao, na kuwashauri wasanii wote kwa ujumla kutumia vyombo vya habari kujiimarisha na kujitangaza.
Kwa  upande wao, wasanii waliopata  tuzo hizo kwa filamu ya “mapenzi ya Mungu” ya  Elizabeth Michael na filamu ya “Kitendawili” ya Single  Mtambalike, wameishukuru Serikali  kwa kuwathamini na kuonesha  ushirikiano katika kazi zao za sanaa, na wameahidi kuendelea  kutengeneza  kazi nzuri za sanaa ili ziweze kuitangaza Tanzania kimataifa.

Naye, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania(TAFF) Saimon Mwakifamba ameishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali  inazofanya katika kusaidia tasnia ya sanaa kwa ujumla na ameahidi kuendelea kushirikiana na  Serikali katika kuendeleza tasnia hiyo kimataifa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.