Neema Kimaro, Mratibu wa kipindi cha Walinde Watoto kutoka True Vision Production akiendelea na maandalizi ya warsha
******************************
Na.Aron Msigwa - MAELEZO.
Maafisa
Maendeleo ya Jamii wanaohitimu mafunzo
katika vyuo mbalimbali nchini na wale waliko kazini wametakiwa kuwa
tayari kufanya kazi vijijini ili kuwawezesha wananchi kuzitumia fursa za
maendeleo zilizoko katika maeneo wanayoishi kukabiliana na changamoto
mbalimbali.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Jamii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.
Enterberth Nyoni wakati akitoa ufafanuzi
kuhusu Utendaji Kazi wa maafisa hao wakati wa kikao kazi cha wakuu wa Vyuo vya
Maendeleo ya Jamii mjini Dodoma.
Amesema
Maafisa Maendeleo popote walipo lazima watambue kuwa wao ni dira na chachu ya
mabadiliko ya kuwafanya wananchi kubadilika kwa kufanya kazi kulingana na
mabadiliko na rasilimali zilizopo katika maeneo yao.
Amesema
kuwa dhana ya Maendeleo ya Jamii ni pana na ikilenga kuwafanya wananchi kutumia
rasimali zinazopatikana katika mazingira yao kujiletea maendeleo akibainisha
kuwa maafisa Maendeleo wanaozalishwa katika vyuo mbalimbali lazima washiriki
kikamilifu katika katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kuwapatia
elimu, ushauri na mbinu mbalimbali za kuondoa umaskini.
Kuhusu
ubora wa kiwango cha taaluma ya maendeleo ya Jamii inayotolewa katika vyuo mbalimbali amesema kuwa ipo haja
ya kuendelea kujenga msingi imara vyuoni na kuandaa vigezo vya kuwapima maafisa
maendeleo ya Jamii kwa kuangalia ufanisi wa utendaji kazi wao wa kila siku.
Amefafanua
kuwa jukumu kubwa la vyuo hivyo pamoja na mambo mengine ni kubadilisha mitazamo
ya wanafunzi walioko vyuoni kwa lengo la kuwafanya kuwa chachu ya mabadiliko na
kuwa msaada kwa wananchi wanaowatumikia.
Kuhusu
mafunzo kwa vitendo Bw.Enterberth amesema kuwa ipo haja kwa wanafunzi walio
katika mafunzo kupangiwa mazoezi kwa
vitendo katika maeneo ya vijijini kwa
kuwa ndiko liliko chimbuko la shughuli Maendeleo ya jamii na kutoa wito kwa
wahitimu hao kuwa tayari kufanya kazi katika mazingira ya vijijini.
Aidha,amesema
kuwa katika kufanya mabadiliko katika taaluma ya maendeleo ya jamii kitaanzishwa Chama au Bodi ya kitaaluma
kusimamia wahitimu wanaomaliza katika vyuo mbalimbali kwa lengo la kupima
uelewa, ubora na viwango kabla ya kuruhusiwa kuitumikia jamii.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu mafunzo kwa maafisa maendeleo ya Jamii walioko kazini amesema
kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo kwa kuhakikisha kuwa
mafunzo rejea kwa maafisa maendeleo ya jamii walioajiliwa yanatolewa ili
maafisa hao waweze kwenda na kasi ya maendeleo na mabadiliko yanayotokea katika
jamii.
Kwa
upande wao baadhi ya Wakuu wa vyuo hivyo wakizungumza kwa nyakati tofauti
kuhusu namna bora ya kuboresha maslahi ya vyuo hivyo hususan kiwango cha
taaluma inayotolewa wameiomba Serikali kwa kushirikiana na wanataaluma husika
kuanzisha Bodi itakayosimamia suala la viwango
na uhakiki wa wataalam wanaohitimu.
Aidha,
wamebainisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wahitimu wa fani ya
Maendeleo ya Jamii imeongezeka jambo linalotoa matumaini ya kukua kwa taaluma
hiyo na kuiomba Serikali kuendelea kuweka vigezo vya udhibiti ili kulinda
viwango vya huduma zinazotolewa.

No comments:
Post a Comment