Na Zainab Nyamka, Dar
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi,
amewataka makocha wanaoshiriki kozi ya ukocha leseni A, kwenda kutumia elimu
hiyo kusaidia na kuendeleza soka la Tanzania.
Malinzi aliyasema hayo jana wakati akifungua kozi hiyo ambayo inashirikisha jumla ya makocha 20 inayofanyika kwenye Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Makocha wanaohudhuria mafunzo hayo.
******************************
“Ndugu zangu makocha nawasihi mnapohitimu kozi hii msiende kuweka vyeti
vyenu ndani bali mkawe chachu ya mafanikio ya soka la Tanzania, kwani kati ya idadi ya makocha
23 wenye leseni A ni makocha saba tu ambao wanafundisha soka”, alisema Malinzi.
Aidha Malinzi alisema kuwa mara tu baada ya kumalizika kwa kozi hiyo, Tanzania itakuwa na jumla ya makocha 43
wenye leseni A jambo ambalo bado ni idadi ndogo ikilinganishwa na Tanzania ambayo
ina jumla ya watanzania milioni 50.
''Kuanzia msimu huu mpya wa ligi makocha
watakaoruhusiwa kuwa na timu za ligi kuu ni wale wenye leseni A tu na kwa daraja
la kwanza ni wenye leseni B na wasaidizi watatakiwa kuwa na leseni C''. alisema Malinzi
Kozi hii itakuwa inaendeshwa na mkufunzi Sunday Kayuni akisaidiana na
Salum Madadi na itakuwa ya mwezi mmoja na itasimama kwa wiki mbili kabla ya kumalizika Novemba, 2016.
Aidha Malinzi amezitaka timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa makini katika usajili wao wa makocha wa kigeni kuanzia msimu wa 2017/18
Amesema, timu hizo zinatakiwa kuhakiki wasifu wa makocha hao na kupeleka ripoti kwa Shirikisho la soka Afrika (CAF) kabla ya kuwapa mikataba ambapo amevitaka vilabu kabla ya kuingia nao mikataba wahakikishe kama wadhifa wao unaendana na vigezo zinavyohitajika Afrika ambapo daraja A ndilo daraja la juu kabisa na endapo CAF hawataridhishwa na viwango hivyo basi makocha hao hawataruhusiwa kufundisha mpira wala kukaa katika benchi la ufundi hapa nchini.
Malinzi amesema kuwa mbali ya walimu hao wa kigeni pia hakuna kocha yoyote mzawa atakayeinoa timu ya ligi kuu kama hana leseni ya daraja A kwani hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha soka la Tanzania na kuzidi ilivyo sasa na makocha wa ligi daraja la kwanza watakaoruhusiwa kuzinoa timu ni wale wenye leseni B huku wenye leseni C wakinoa timu za daraja la pili.
"Tutahakikisha kuanzia msimu wa 2017/18 makocha wote watakaozinoa timu za ligi kuu wanakuwa na daraja A pia makocha wa kigeni wataangaliwa zaidi ili kuondokana na vitendo vya udanganyifu", alisema Malinzi.
Aidha aliwataka wanawake kujitokeza katika mafunzo hayo ili kusaidia harakati za kukuza soka la wanawake nchini.
Kwa upande wake Mkufunzi mwandamizi wa CAF, Sunday Kayuni alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kukubwa walimu kuwa na timu zenye wachezaji wazuri na wenye uwezo mkubwa na endapo jambo hilo litafanikiwa basi ni wazi kuwa Tanzania ipatapa vijana wengi zaidi watakaocheza soka la kulipwa na kuzidi kupeperusha vema bendera ya nchi kupitia soka.
"Ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya ambayo ndiyo yanayotoa walimu wenye sifa za juu kabisa Afrika, Tanzania itaweza kuwa vizuri kwa upande wa soka na kuleta mabadiliko", alisema Kayuni.
Picha ya pamoja.



No comments:
Post a Comment