Habari za Punde

*NEY WA MITEGO APIGWA PINI NA WIMBO WAKE WA 'PALE KATI PATAMU'


BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati patamu’ ulioimbwa na Msanii Emannuel Elibariki maarufu kama Ney wa Mitengo kutokana na kile kilichoelezwa ni ukiukwaji mkubwa wa maadili.
Taarifa ya BASATA iliyopatikana leo Julai 16, 2016 jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Ktibu Mtendaji wa Baraza hilo Godfrey Mngereza imesema, msanii huyu amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka maadili.
Mngereza amesema katika taarifa yake kali kwa vyombo vya habari kuwa kazi zake zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Kufungiwa kwa wimbo huo kuna kuja muda si mrefu tangu kufungiwa kwa wimbo mwingine uitwao “Chura” ulioimbwa na Snura.
“Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.” Alisema
Mngereza amesema, Ney wa Mitego ameitwa na kuonywa mara kadhaa kutokana na BASATA ilichokiita tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ney aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo.
Hata hivyo BASATA kupitia kwa Katibu huyo Mtendaji imesema “Ney wa Mutego kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine.”
“Wimbo wa Pale Kati patamu kwa sasa uko mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama.” Alisema Mngereza katika taarifa yake
Kwa mantiki hii BASATA imesema haitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa na wasanii genge la wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa jamii, taarifa hiyo imeendelea kusema
Kufuatia hatua hiyo, baraza hilo limetoa maelekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuufungia rasmi wimbo wa “Pale Kati Patamu” na hauruhusiwi kutumika kwa namna yoyote.
Aidha pamoja na adhabu ya kufungia wimbo huu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake..
BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.