Na Zainab Nyamka, Dar
KUFUATIA kuibuka kwa habari za uzushi na tetesi zinazodai kuwa kocha mpya wa timu ya Azam FC Zeben Hernandez, kutokubali kiwango cha Naodha na shambuliaji wa timu hiyo John Bocco, uongozi wa timu hiyo ubeibuka na kukuanusha habari hizo na kusema kuwa mwalimu huyo bado hajatoa tathmini yake kuhusu wachezaji wanaostahili kubaki kikosini.
Uongozi huo kupitia kwa katibu mkuu wake Sadi Kawemba umesema kuwa kocha huyo anatarajiwa kutoa tathmini ya timu hiyo toka alipopokea mikoba ya kukinoa rasmi Kikosi hicho Jumatatu ya wiki ijayo na anashangazwa na taarifa hizo kwani kama uongozi hawajapokea taarifa zozote kutoka kwa mwalimu inakuaje watu wa nje wanaongea kitu wasichokijua.
Azam waliingia kambini mwanzoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kujiweka sawa na kujiandaa kwa msimu ujao wa ligi kuu ikiwa ni pamoja na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kama majaribio kwa wachezaji wao waliokuja katika majaribio.
Baada ya kuanza na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Ashanti united katika mchezo wao wa kujipima nguvu na majaribio kwa wachezaji wapya, sasa timu ya Azam FC inatarajia kucheza mechi nyingine za kirafiki na majaribio kwa wachezaji wao wapya kabla ya kuanza rasmi kwa mechi zao za kifariki.
Kuelekea msimu ujao timu hiyo imepanga kuwa na kikosi bora zaidi ili kutimiza adhma yao ya kunyakua ubingwa baada ya Yanga kutwaa taji hilo misimu miwili mfululizo.
Naye Afisa habari wa timu hiyo Jaffar Idd Maganga, alisema kuwa baada ya kucheza na kupata ushindi dhidi ya Ashanti sasa wanaendelea na michezo mingine ambapo mchezo wa pili wamewaalika Friends Rangers, ambapo michezo hiyo itaendelea kupima uwezo wa wachezaji wao wapya ambao wamekuja ndani ya Azam kwa ajili ya majaribio.
Amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na wachezaji hao kuja kwa nyakati tofauti hivyo wale watakaofuzu majaribio watakuwa nao katika michezo mingine hasa ya kirafiki ya kimataifa, "Mwalimu aliomba mechi za kirafiki za mapema ili kuangalia uwezo wa wachezaji waliokuja katika majaribio huku tukiamua timu yetu icheze na timu za daraja la kwanza kwani zimekuwa kambini kutokana na kushiriki mashindano mbalimbali pia ni nzuri kwani zimekuwa zikitupa wakati mgumu." alisema Jaffar

No comments:
Post a Comment