Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai kwa jamii kupiga vita mila na
tamaduni potofu zinazosababisha kuwepo kwa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa
watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 13 hadi 18.
Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai hiyo wakati
alipokuwa akizindua maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani iliyofanyika
katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo
mengine ameiomba jamii na Mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali
kushirikiana kwa pamoja kutokomeza mila hizo.
Amesema kuwa kuwa mfumo dume ndio changamoto
kubwa inayowakwaza watoto wa kike kuanzia ngazi ya kaya ambapo kazi za ndani
kama za kuosha vyombo, kufagia na kuhudumia nyumba kwa ujumla hufanywa na mtoto
wa kike, hali hiyo humpotezea muda mtoto wa kike hatimae kupunguza ushiriki
wake katika elimu na mambo mengine ya maendeleo.
" Takwimu zilizotokana na utafiti
uliofanywa mwaka 2014 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ( NBS) juu ya Watu wenye
Uwezo wa Kufanya Kazi zimeonyesha kuwa asilimia 43.8 ya watoto wa kike
hushiriki katika shughuli za nyumbani zisizo za kiuchumi na kiwango cha
wasichana walioajiriwa ni asilimia 47.5 wakati wavulana ni asilimia 52.5 hivyo,
tuna kila sababu ya kumkomboa mtoto wa kike", Amesema Mhe. Ummy.
Amesisitiza kuwa silaha kubwa ya kumkomboa mtoto
wa kike ni kumpa elimu bora na ya kutosha pia kupinga mila na tamaduni potofu
juu ya watoto hao kwakua ndizo zinazoleta changamoto nyingi zikiwemo za ndoa na
mimba za utotoni pamoja na fursa ndogo za kupata elimu na ajira.
Aidha,waziri huyo ametoa wito kwa Watendaji wa Serikali
ngazi ya Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu
ya kumlinda mtoto wa kike na kuwekeza katika maendeleo yake pia waendelee
kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Elimu inayotoa katazo la kuoa au
kuolewa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 19.
Amelipongeza Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) kwa jitihada zao za kuwajengea
wasichana uwezo wa kujitambua na kufahamu masuala mbalimbali ya kijamii
yanayoendelea pia ametoa wito kwa wadau kuangalia namna ya kuwafikia wasichana
wengi waliopo maeneo ya vijijini.

No comments:
Post a Comment