Jengo la
kiwanja cha ndege cha Nduli cha mkoani Iringa.
***************************************
SERIKALI ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Rais Dk John Magufuli imetenga kiasi cha sh. Bil. 100 katika bajeti ya mwaka
2016/17 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege
nchini.
Rais Dk. Magufuli alisema hayo juzi
katika sherehe za uzinduzi wa ndege mbili za Shirika la ndege la Tanzania
(ATCL) aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na serikali, kwenye
Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo viwanja hivyo
vitaboreshwa ili kuwezesha ndege hizo kutua bila wasiwasi.
Mhe. Rais akifafanua zaidi, alisema , kiwanja
cha ndege cha Nduli kilichopo umbali wa kilometa 13 Kaskazini Mashariki mwa
Manispaa ya Iringa, ambacho kipo kwenye kiwango cha lami kitakarabatiwa, ili
ndege hizo zitue na kupaa bila tatizo.
Dk. Magufuli alisema, kiwanja cha Nduli
Iringa ni kiunganishi kikubwa na JNIA na kitatumika kupeleka watalii
wanaokwenda kutembelea mbuga ya wanyama ya Ruaha, wakitokea Mataifa mbalimbali
duniani.
Alisema mbali na kiwanja hicho cha
Nduli, pia kiwanja cha Musoma kitawekwa lami, ili nacho kiwe moja ya maeneo
ndege hiyo itakwenda, na kurahisisha usafiri wa watalii watakaokwenda kwenye
mbuga ya wanyama ya Serengeti. Kwa sasa kiwanja cha Musoma kipo katika kiwango
cha changarawe na kinatumika kwa ndege mbalimbali kutua na kupaa.
Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha
ndege cha Nduli, Bi. Hannah Kibopile, kiwanja hicho kinapokea ndege ndogo zaidi
ya saba zenye uwezo wa kubeba abiria 13, na kati ya hizo tatu zipo kwenye
ratiba maalum ya kila siku na zilizosalia ni za kukodishwa na nyingine
zinakwenda mbuga ya wanyama ya Ruaha.
Bi. Kibopile alisema ndege zinazotua
kwenye kiwanja hicho zinatoka Jijini Dar es Salaam, Sumbawanga, Songea na Mbuga
ya Ruaha.
Naye Kaimu Meneja wa Musoma, Bi. Faraja
Mayugwa amesema kiwanja hicho kinapokea ndege zaidi ya nne kwa siku na nyingi
zinakuwa za kukodi zinazopeleka watalii mbugani.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli
alisema “Hii ndege inaweza kutua katika kiwanja cha aina yeyote; na serikali
itaendelea na ukarabati wa viwanja vya ndege vya pembezoni, ili viwe katika
kiwango, ambacho ndege hizi zitatua na kuruka bila wasiwasi,”.
Akifafanua zaidi Dk. Magufuli alisema
serikali inatarajia kununua ndege nyingine kubwa mbili zenye uwezo wa kubeba
abiria 160 na 242, ambazo zitaanzia safari zake kwenye JNIA kwenda sehemu
mbalimbali duniani kama China au Marekani moja kwa moja, ikiwa ni lengo la
kupata abiria hao, ambao wengi wao watakuwa watalii wanaokuja nchini kutembelea
vivutio mbalimbali. Bombardier inauwezo wa kubeba abiria 76.
Naye Waziri wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof Makame Mbarawa awali wakati akimkaribisha
Mhe. Rais kuzungumza na wananchi katika ghafla hiyo ya uzinduzi wa ndege, alisema
kwa kuanzia ndege hizo zitatua kwenye viwanja 11 vya ndege, ambavyo ni Kiwanja
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro (KIA), Zanzibar (AAKIA),
Mwanza, Dodoma, Arusha, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya na Mtwara. Pia ndege hiyo itakwenda Comoro.
Mhe. Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa
kuangalia viwanja vingine vya ndege,
ambavyo ndege hizi zitakwenda.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO - TAA

No comments:
Post a Comment