Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
akihutubia mkoani Dodoma katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi
wapatao 187 watakaofanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa
mwaka 2016 unaotarajia kuanza nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
Baadhi ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo mkoani Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya kina kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akizungumza leo mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
Mratibu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 Bi. Mariam Kitembe wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akimkabidhi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kiasi cha Shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000) zilizochangwa na wadadisi wa Utafiti huo kwa ajili ya waathirika wa Tetemeko lililotokea mkoani Kagera hivi karibuni. Mhe. Ummy Mwalimu amekabidhiwa fedha hizo wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo mkoani Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 mara baada ya kufunga mafunzo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 leo mkoani Dodoma. Picha na Veronica Kazimoto.
****************************
Na.
Emanuel Ghula, Dodoma
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza
Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kutoa ruhusa kwa manesi ambao ni wadadisi
wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 ili kufanya
utafiti huo.
Akizungumza
leo katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi hao iliyofanyika mkoani
Dodoma, Waziri Ummy amesema utafiti huu ni wa muhimu sana hivyo Makatibu Tawala
hawana budi kuwaruhusu manesi hao waliopata mafunzo kufanya utafiti huo.
“Ninawaagiza
Makatibu Tawala wote nchini kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa manesi mliopo hapa
leo ili muweze kulisaidia taifa letu kwa kutuletea takwimu sahihi
zitakazosaidia katika kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo hususani
katika suala zima la afya”, ameagiza Mhe. Ummy Mwalimu.
Amefafanua
kuwa, takwimu hizi zitasaidia kuboresha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali
za kusogeza huduma zinazohusiana na VVU kama vile huduma za upimaji wa VVU bure
katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali, kutoa huduma ya kupunguza
maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) pamoja na utoaji wa dawa za
kupunguza makali ya VVU zijulikanazo kama ARV.
“Utafiti
huu ni wa kipekee ukilinganisha na tafiti zingine zilizofanywa zinazohusu
UKIMWI kutokana na kujumuisha upimaji wa homa ya ini ambao umekuwa tishio
katika baadhi ya nchi barani Afrika”, amesisitiza Mhe. Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi wote nchini kutoa ushirikiano kwa wadadisi
watakaopita katika kaya mbalimbali zilizochanguliwa kwa ajili ya kufanya
utafiti huu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa
amesema utafiti huu utahusisha watu wote kwenye kaya zipatazo elfu kumi na sita
(16,000) zilizochaguliwa kitaalam na kuwafikia watu wazima wapatao elfu
arobaini (40,000) na watoto zaidi ya elfu nane (8,000).
Dkt.
Chuwa ameeleza kuwa, takwimu hizi zitaisaidia Serikali katika kupanga na
kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazohusu sekta ya afya nchini
hususani upatikanaji wa huduma za afya.
Wadadisi
wapatao 187 ambao ni manesi kutoka hospitali mbalimbali nchini, wamemaliza
mafunzo ya Utafiti wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI ambao unatarajia kuanza
wiki ijayo.
Utafiti
wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI utahusisha upimaji wa UKIMWI, maambukizi
mapya na wingi wa VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU, wingi wa chembechembe
za kinga mwilini (CD4 T-cell count), kiwango cha usugu wa dawa za ARV, kiwango
cha maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini (Hepatitis B na C).






No comments:
Post a Comment