SHIRIKISHO
LA MICHEZO YA WIZARA NA IDARA ZA SERIKALI
TAARIFA
KWA UMMA
KUAHIRISHA
MICHEZO YA SHIMIWI KWA MWAKA 2016
Shirikisho la
Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) katika Kalenda ya mwaka 2016
ilipanga michezo ya SHIMIWI ifanyike mkoani Dodoma kuanzia tarehe 14-27
Novemba, 2016.
Kama mnavyofahamu
hivi karibuni Taifa limekumbwa na janga la tetemeko la ardhi Mkoani
Kagera. Janga ambalo limesababisha vifo,
limeacha familia nyingi kukosa makazi.
Tetemeko hili limeleta madhara makubwa. Taasisi, Mashirika, nchi
mbalimbali na watu binafsi wameguswa kwa ajili ya kuchangia waathirika wa
tetemeko ili kukabiliana na madhara yaliyotokea. 

Katika kutimiza
dhamira ya kuleta maendeleo katika Taifa Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuchukua hatua
mbalimbali ili kuleta ufanisi. Zikiwemo
kuahirisha Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru ili fedha ambazo zingetumika
zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na vile vile imeelekeza kuhakikisha azma
ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma inatimizwa.
Majukumu yote niliyoyataja
yanategemea Mapato ya Serikali. Vile
vile gharama za kuendesha Michezo ya SHIMIWI kwa kiasi kikubwa zinatokana na
Bajeti ya Serikali. Tunapenda kuwaarifu
Wananchi, Wanamichezo wote na Watumishi wa Umma wote kuwa kwa kuzingatia
majukumu yote ambayo Taifa inayatekeleza kwa sasa SHIMIWI imeamua kuunga mkono
kwa kuahirisha michezo ya SHIMIWI kwa
mwaka huu 2016 ili kushirikiana kuelekeza nguvu pamoja na makundi mengine ya kijamii
wakiwemo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu hayo. Tunawashauri watumishi wote waendelee kufanya
mazoezi kwa ajili ya kujenga afya zao kupitia ushiriki wa pamoja kwenye Bonanza
la Wafanyakazi wa Umma katika maeneo yao katika siku za mwisho wa wiki.
Vile vile naomba
nitumie fursa hii kusisitiza vilabu wanachama vihakikishe vinalipa
ada ya mwaka kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka utakaofanyika
Januari, 2017. Hadi sasa ni timu chache
zimekwishalipa. Kumbukeni kwamba kwa
mujibu wa katiba ya SHIMIWI wanachama watakaoshiriki kwenye Mkutano Mkuu wa
mwaka ni wale waliolipa ada ya mwaka.
Daniel Mwalusamba
MWENYEKITI
- SHIMIWI - TAIFA
11
Oktoba, 2016
KWA
PAMOJA MAKUNDI YOTE YA KIJAMII
TUSHIRIKIANE
KULIJENGA TAIFA LETU TANZANIA
MUNGU
IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA
No comments:
Post a Comment