Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt. Rehema J. Nchimbi (wa kwanza kushoto) akiwa ofisini kwake alipotembelewa
na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano
vijijini kwenye mkoa huo
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Willy Quambalo (wa kwanza kulia) akisisitiza jambo kwa wataalamu wa kampuni ya simu ya Halotel wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini walipokuwa kwenye kijiji cha Kijima kilichopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Msimamizi wa kampuni ya Halotel wa mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Benedict Kishusha (wa pili kushoto) akifafanua jambo mbele ya kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye kijiji cha Kijima kikichopo mkoa wa Mwanza.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Abbasi Hassani Mwinyi (wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa wataalamu wa kampuni ya Vodacom (hawapo pichani).
Msimamizi wa kampuni ya simu ya Vodacom wa Mkoa wa Dodoma Bwana Bwana Benedict Maro akifafanua jambo mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani) wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini katika kijiji cha Idondandoye kilichopo wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Aliye katikati ni Mkuu wa Idara ya Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Bwana Albert Richard.
********************************
Kamati ya Bunge ya
Miundombinu iko kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu, ufikishaji
na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye maeneo ya vijiji
mbalimbali nchi nzima ikiwa ni moja ya jukumu la Kamati hiyo ya kusimamia na
kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
ya kujenga miundombinu ili kukuza uchumi wa taifa letu, kuchangia pato la taifa
na kuiwezesha Serikali kuhudumia wananchi wake.
Hayo yameelezwa na
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson
Mwkasaka wakiwa kwenye ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma za
mawasikiano vijijini kwenye kijiji cha
Kijima kilichopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza. Mhe. Mwakasaka amesema kuwa
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imwekeza kwenye
kampuni ya simu ya Halotel ili iweze kufikisha huduma za mawasiliano vijijini a
kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili wananchi wa vijijini waweze
kutumia huduma hizo na kunufaika nazo sawa na wanachi waishio mijini.
Naye Msimamizi wa Kampuni ya simu ya Halotel
wa Mkoa wa Mwanza na Simiyu Bwana Benedict Kishusha amesema kuwa Halotel ina
watumiaji wachache kwenye vijiji mbalimbali nchini ambako kampuni hiyo imejenga
minara na wananchi waishio maeneo hayo wana uwezo mdogo wa kiuchumi wa kutumia
huduma za mawasiliano kama vile kununua muda wa maongezi ili kufanikisha azma
ya Serikali ya ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
“Halotel imekuwa ikiwapatia wananchi simu za mkononi bure bila ya kuwauzia ili
waweze kuwasiliana na kutumia huduma nyingine za mawasiliano,” amesema
Kishusha. Ameongeza kuwa kijiji cha Kijima kina takribani ya watu 2,000 na
mnara huo umewashwa na kuanza kutumika mwezi Julai mwaka 2015.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka ametoa rai kwa kampuni
ya simu ya Halotel kutangaza huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja
na kuweka mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi. Pia
ameongeza kuwa waendelee kujitangaza hasa kwenye maeneo ya vijijini walikojenga
minara yao ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano vijijini kama vile
kutuma na kupokea fedha kwa kuwa hamna huduma za kibenki kwenye maeneo ya
vijijini na wananchi wanategemea huduma hiyo kupitia kampuni ya simu ya
Halotel. Pia ameongeza kuwa Halotel
waendelee kutangaza huduma zake za kutoa na kuweka fedha pamoja na kuweka
mfumo wa matumizi ya data ya 3G kwani ndizo zinawavutia wananchi.
Akizungumza kwenye
ziara hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Kijima wilayani Misungwi mkoani
Mwanza, Mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe. Ritha Kabati amesema kuwa wananchi wengi
wanahitaji huduma ya kuweka na kutoa fedha kwani ndiyo huduma muhimu kwao. Kabati
alisema wananchi wengi walioko vijijini hawatambui kama Haloteli inatoa huduma
ya kutoa na kuweka fedha hivyo hutumia mitandao mingine inayopatikana huduma
hiyo. "Wananchi wengi waliopo vijijini hawatambui kama kuna Halopesa
wanachokijua ni M-pesa wakati huduma hii ni muhimu kwa kuwa watoto, ndugu na
jamaa walioko mjini huwatumia fedha kwa njia ya simu za mkononi hivyo
kukosekana kwa huduma hii kunachangia watu wasiitambue," amesema Rita
Kabati.
Pia Mjumbe wa Kamti
hiyo Mhe. Mussa Ntimizi alisema serikali imetoa ruzuku kwa kampuni za simu
lengo ni kueneza huduma za mawasiliano hivyo baada ya ujenzi wa minara mnatakiwa
kuweka promosheni mbalimbali na matangazo ya kutosha kujitangaza. "Haloteli
mtengeneze matangazo ya kutosha ili watu waitambue kwani Serikali imeweka
fedha za kutosha ili wananchi wapate huduma zote muhimu. Natambua kwamba huduma
ya kuweka na kutoa fedha (Halopesa) imeanza kutoa huduma lakini ipo zaidi mjini
hivyo mnapaswa kuitangaza na huku vijijini," alisema Ntimizi. Pia amesema
kama ambavyo Haloteli inafanya vizuri katika masuala ya data mijini, wanapaswa
kuweka huduma hiyo vijijini kwani suala la mawasiliano limekuwa hivyo
wasitegemee kuwa wanakijiji hawatumii data. "Kwa sasa wananchi
wanapendelea zaidi data katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook,
Instagram na WhatsApp hivyo msifikiri kwa kuwa huku ni vijijini basi hawatumii
hapana, mnatakiwa muweke data nzuri kisha muangalie watumiaji wako wengi kiasi
gani," alisisitiza.
Mwanakijiji wa Kijima,
Bi. Hellen Michael alisema kuwa katika kijiji hicho wanatumia zaidi mtandao wa
Vodacom na kwamba wengi wanatambua huduma za M-Pesa na sio Halopesa. Alisema
huduma hiyo ya kuweka na kutoa fedha kwa Haloteli imeanza miezi minne iliyopita
na kwamba wanakijiji wanapenda kutumia huduma hizo zaidi. “Wananchi wanafurahia
na kutumia simu ya kampuni ya Halotel bali tunaiomba itoe huduma za kuweka na
kutoa pesa,” amesema Bi. Hellen Michael.
Naye Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga amesisitiza kuwa kampuni ya
simu ya Halotel itoe huduma za data kwa wananchi waishio vijiji mbalimbali
walikojenga minara na sio huduma za simu za sauti tu ili wananchi waweze kupata
huduma za mawsilaino ya sauti na data kupitia kampuni hiyo kama ilivyo kwa
wananchi waishio mijini.
Msimamizi wa Kampuni
ya Haloteli mkoa wa Mwanza na Simiyu, Bwana Benedict Kishusha alisema kuwa
mnara huo uliwashwa Julai, 2015 ambao unahudumia vitongoji 23 vya kijiji
hicho. Kishusha alisema changamoto mojawapo ni watumiaji wachache wa mitandao
ya simu katika kijiji hicho unaosababishwa na uwezo mdogo wa kupata
huduma za mawasiliano ikiwemo ununuaji wa vocha. Alisema wanajitahidi kuelimisha watu kutumia
mtandao huo ikiwemo kufanya matangazo mbalimbali na kuwapatia bure kadi za simu
na muda wa maongezi. "Huduma ya Halopesa imezinduliwa hivi karibuni na
kijiji hiki kimeanza kutumia huduma hiyo miezi mitatu iliyopita. “Katika mnara huu wanatumia data ya 2G kwani
hatuwezi kuweka 3G kwa sababu watumiaji wake ni wachache hivyo inaongeza
gharama," alifafanua Kishusha. Pia alieleza kuwa awali, walifunga
data ya 3G lakini kijiji hicho na vingine waliona watumiaji wa simu za
mkononi za kutumia data za 3G ni wachache na mfumo wao unasoma hivyo ambapo
iliwalazimu kutoa huduma hiyo na kupeleka vijiji vingine na kuacha huduma ya
data ya 2G ikiendelea kufanya kazi na kutumika kwenye kijiji hicho.
Naye Kaimu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu, Mhe. Emmanuel Mwakasaka
alisisitiza kuwa ni vyema kampuni hiyo kuzingatia kutoa huduma zote ili
wananchi waweze kunufaika na mawasiliano sio tu ya kuongea. Pia alizitaka
Kampuni za simu zote zinazotumia huduma za mawasiliano kote nchini
kuhakikisha zinashiriki katika kusaidia huduma za jamii. Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi wa Haloteli mkoa wa Mwanza, Francis Mafuru alisema
wanajitahidi kutoa huduma za kijamii licha ya kwamba wananchi hao wapatao 2,000
hawatumii vocha zaidi ya shilingi 500 hali inayoongeza gharama za uendeshaj wa
kampuni hiyo ya simu. "Tunaamini wateja wetu wataongezeka kwani
tumejipanga vizuri kuwahudumia katika masuala ya fedha na data," alisema
Mafuru.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment