KAMPUNI ya
Lino International Agency Limited, waandaji wa mashindano ya urembo ya Miss
Tanzania tunapenda kuwajulisha wapenzi, mashabiki na wadau wa tasnia ya urembo
kwamba hakutakuwa na Fainali za Taifa za shindano la Miss Tanzania kwa mwaka
2017.
Sababu kubwa
za kuahirishwa kwa Fainali hizi ni ukosefu wa Wadhamini ambao kwa njia moja au
nyingine huwezesha kufanyika kwa mashindano hayo kwa kulipa gharama mbalimbali
ikiwemo zawadi za washiriki n.k.
Aidha
kuchelewa kupata kibali cha kuanza mchakato wa Miss Tanzania 2017 pia
kumechangia kukosa Wadhamini kutokana na muda kuwa mfupi. Kibali cha kuendesha
mashindano ya Miss Tanzania 2017 kimetolewa na Basata mwezi Septemba 2017.
Washindi wa
Mikoa na Kanda ambao tayari wameshinda katika sehemu mbalimbali ambao wamefanya
mashindano yao kwa mwaka 2017 watashiriki Fainali za Taifa kwa mwaka ujao wa
2018 katika tarehe na mwezi ambao tutawajulisha hapo baadae.
Baadhi ya
Mikoa na Kanda mbalimbali ambao hawakuweza kufanya mashindano yao kwa mwaka
2017 kutokana na changamoto za udhamini, tunawapa muda wa kujipanga upya hadi
mwezi Mei 2018 wawe wamefanya mashindano yao ili kutoa nafasi kwa Fainali za
Taifa kufanyika.
Aidha
tunapenda kuchukua fursa hii kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini
mashindano ya Miss Tanzania 2018 ili
kutoa fursa kwa wasichana washiriki ambao ndio walengwa wa mashindano haya.
Kamati ya
Miss Tanzania inawataka Mawakala wote wa Miss Tanzania kufuata Kanuni, Sheria
na Taratibu za Mashindano ikiwa ni pamoja na kusajiliwa na kulipa ada husika
Baraza la Sanaa la Taifa, kuandaa shindano lenye hadhi na kutoa zawadi kwa wakati.
Mawakala pia
wanatakiwa kuwa na ofisi na mawasiliano yanayoeleweka.
Wakala
ambaye hatotimiza masharti hayo, shindano lake halitotambuliwa na hivyo
kuwanyima fursa washiriki wa mashindano haya.
Uongozi wa
Kampuni ya Lino International Agency Limited tunapenda kutoa shukrani zetu za
dhati kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Baraza la
Sanaa la Taifa (BASATA) kwa ushirikiano wao ambao wamekuwa wakitupatia kila
mara tunapohitaji kufanya hivyo.
HIDAN .O. RICCO.
AFISA HABARI.
0673 019112
No comments:
Post a Comment