Habari za Punde

TRC KUFUNGA NJIA YA TRENI KWA SAA 72 KILA WIKI

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa kwenye Viwanja vya Julius Nyerere Dar es Salaam, jana akitangaza kuhusu kufungwa kwa njia ya Reli ya Kati kwa saa 72 ili kupisha ukarabati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka ambapo njia hiyo itakuwa ikifungwa mara tatu kwa wiki kuanzia julai 13 mwaka huu. 
*************************
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kufunga njia ya Treni ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga kwa saa 72 kila wiki ambayo ni sawa na siku tatu kwa wiki ili kufanikisha ukarabati wa reli hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa, alisema kuwa ukarabati huo wa takribani kilometa 970 unaotarajia kuanza Julai 13 mwaka huu utachukua miezi mitatu zoezi ambalo kukamilika kwake kutaingiza faida mara dufu ya usafiri huo na kwa Taifa.
“Waandishi wa Habari na Watanzania kwa ujumla, TRC sasa tunakuja kuimarisha miundombinu ya Reli, tunafanya hivi kwa kuwa tunafahamu mnahitaji huduma hizi, tunaomba mtuvumilie kwa siku ambazo tutafunga njia hizi”alisema Kadogosa.
Aidha alisema kuwa ukarabati huo ni pamoja na kubadilisha Mataluma na Reli kutoka ‘Pound 60 hadi Pound 80’ na kuunga maungio ya reli kwa umeme  ‘Flash Butt Welding’ ili kupunguza wizi wa vifungashio uliokuwa ukitokea siku za nyuma kwa kufungua bolt za viunganishio vya reli ‘fish plate’ katika maungio ya reli.
Alizitaja faida za ukarabati huo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa Speed ya Treni kutoka kilometa 35 kwa saa mpaka kilometa 75 kwa saa pamoja na kuongeza uwezo wa ubebaji mizigo kwa Exeli moja kutoka Tani 13 hadi 18.
‘’Baada ya kukamilika ukarabati huu Treni zetu zitaweza kubeba mizigo mingi zaidi kwa wakati mmoja, kwa haraka na usalama zaidi na pia itapunguza ajali za mara kwa mara,
Lakini pia itaboresha mawasiliano na ishara za kuongezea Treni kwa kuweka mfumo wa kisasa ujulikanao kama ‘Train Warranty System’ ili kuondoa usumbufu wa mawasiliano kutoka kituo kimoja hadi kingine
Alibainisha kuwa ukarabati mwingine wa njia ya Reli kutoka Tanga kwenda  Arusha ulianza mapema mwaka huu ambapo njia hiyo itaanza kutumika mwezi Desemba mwaka huu.
“Ndugu zangu wa mikoa ya Kaskazini mtaanza kunufaika na usafiri wa treni ya Abiria kuanzia Desemba mwaka huu, yaani Sikukuu zaKrismas na Mwaka mpya mtaenda nyumbani na Treni ya Abiria ya TRCälisema Kadogosa.
 Akizungumzia ujenzi wa Reli ya Standard Gauge inayoendelea kujengwa Nchini Kadogosa alisema kwa awamu ya kwanza kutoka Dar Es Salaam kwenda Morogoro ujenzi huo umefikia asilimia 56.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, akisikiliza maelezo kutoka kwa fundi simu wa shirika hilo, John Mandari, kuhusu simu zinazotumika kwa mawasiliano katika Stesheni za Treni wakati alipotembelea katika Banda lao la Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, leo. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.