Habari za Punde

HUU NDIYO FULL USAJILI WA YANGA

UONGOZI wa Yanga umesema kwa asilimia 100 wamekamilisha usajili uliotakiwa kwa maelekezo ya kocha wao, Nasredine Nabi lakini wanasaka mshindani wa Sureboy mwenye uwezo wa kusukuma mashambulizi.
Yanga ilianza kwa kuwaongezea mikataba wachezaji wao Farid Mussa, Kibwana Shomari, Zawadi Mauya, Bakari Mwamnyeto kisha wakageukia upande wa nyota wapya kwa kumsajili Lazarous Kambole (huru) na wanatajwa kumalizana na beki Joyce Lomalisa (huru) pamoja na Azizi Ki kutoka Asec Mimosas.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mbatha alisema usajili wao kwa kiasi kikubwa umeenda vizuri na imebaki nafasi moja ingawa habari za chini chini inaelezwa .wanajangwani hao bado wanaendelea kusaka saini ya Simon Msuva.
“Sisi tumekamilisha usajili wetu kwa kiasi kikubwa na eneo lililobaki ni kiungo mwenye uwezo wa kucheza katikati (Boksi kwa Boksi) na ndio tutamalizia hapo,” alisema Senzo ambaye ni raia wa Afrika ya Kusini.
Senzo alisema usajili wa msimu ujao wanaangazia zaidi michuano ya Kimataifa na ndio maana wametulia kuhakikisha unaenda sawa ili watimize malengo yao.
Akizungumzia kumpa mkataba mpya kocha wao Nabi na benchi la ufundi, alisema jambo hilo linamalizika siku chache zijazo.
“Kweli lakini jambo lake linamalizika ndani ya wiki hii na tulishafanya mazungumzo,” alisema Senzo huku akijiamini na kukata mzizi wa fitina kocha huyo anaweza kutimkia kwa watani zao wa jadi Simba.

HATMA YA YASSIN KWA NABI
Senzo alisema kwa asilimia kubwa wachezaji wote wa Yanga wana mikataba kwa wale waliomaliza tayari waliongezewa lakini upande wa mchezaji ambaye hajaongezwa wanafahamu.
Alipoulizwa kuhusu beki Yassin Mustapha ambaye bado hajaongezwa mkataba alisema; “Kweli huyo bado lakini mwenye maamuzi ya mwisho ni kocha.”
Yassin hajawa na wakati mzuri ndani ya Yanga baada ya kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hali iliyomfanya Nabi amtumie Farid Mussa au Kibwana kucheza kama beki wa kushoto.
Beki huyu alisajiliwa misimu miwili nyuma akitokea Polisi Tanzania baada ya kuonyesha kiwango kizuri.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.