Habari za Punde

TAIFA STARS, UGANDA NI MTANANGE WA KIBABE KESHO

Na Raul Majuto

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kesho Jumanne Machi 28 itacheza mchezo muhimu dhidi ya Uganda (The Cranes) katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) iliyopangwa kufanyika mwakani nchini Ivory Coast.

Mchezo huo wa Kundi F umepangwa kuanza saa 2.00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na wachezaji wa Taifa Stars wamepania kuibuka na ushindi.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika mjini Ismailia, Misri, Taifa Stars ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva aliyepokea pasi safi ya Dickson Job.

Ushindi huo umeifanya Taifa Stars kushika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi nne huku Algeria ikiwa ya kwanza kwa kujikusanyia pointi tisa (9) na Niger ikiwa katika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi mbili (2). Uganda inashika mkia katika kundi hilo kwa kuwa na pointi moja.

Kutokana na msimamo huo, Taifa Stara inasaka ushindi kwa namna yoyote katika mchezo huo ili kujihakikishia asilimia 95 za kufuzu katika mashindano ya Afcon ya Ivory Coast yaliyopangwa kufanyika mwezi Januari na Februari mwakani.

Kimahesabu, ushindi dhidi ya Uganda katika pambano hilo utaiwezesha Taifa Stars kukusanya pointi saba ikiwa na mechi mbili mkononi na itahitaji pointi mbili pekee ili kufuzu kwa fainali za Afcon kwa mara ya tatu katika historia.

Matokeo ya sare pia yataiongezea Taifa Stars nafasi ya kufuzu ambapo itahitaji ushindi dhidi ya Niger katika uwanja wa nyumbani mwezi Juni mwakahuu.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema kuwa wanatarajia kupata ushindani mkali kutoka kwa Uganda, lakini wachezaji wake wamehapa kufanya vyema katika mchezo huo.

“Itakuwa mechi ngumu kwani kila timu iahitaji ushidni ili kuweka matumaini hai ya kufuzu.Waganda watakuja tofauti katika pambano hilo na tunafahamu hilo. Wachezaji wangu wako katika morali ya hali ya juu na wako tayari kutoa matokeo bora kwenye uwanja wa nyumbani,” alisema Morocco.

Kwa upande wake, kocha mkuu wa The Cranes ya Uganda Milutin Sredojevic maarufu kwa jina la Micho pia analenga matokeo bora dhidi ya Tanzania kwenye pambano hilo.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza Taifa Stars kwa ushindi wa mchezo wa kwanza na ameahidi kutoa Sh10 milioni kwa bao lolote litakalofungwa katika mchezo huo na mechi zilizobakia.

Wakati huo huo; serikali imetoa jumla ya tiketi 20,000 zitakazotolewa kwa mashabiki wa soka kutazama mechi hiyo.

Katika tiketi hizo, Rais Samia ametoa tiketi 7,000 huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akichangia tiketi 2,000 na Wizara ya Utamaduni. Sanaa na Michezo imetoa tiketi 11,000.

Mchezo huo ungechezeshwa na mwamuzi wa Ivory Coast Ibrahim Kalilou Traore ambaye atasaidiwa na Adou Hermann Desiré N’goh pia kutoka Ivory Coast na mwamuzi wa DR Congo Quattara Nouho. Mwamuzi wa akiba ni pia ni raia wa Ivory Coast Clement Franklin Kpan.


Feisal Salum Toto, akiwa katrikati ya msitu wa wachezaji wa Uganda,

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.