Habari za Punde

VIONGOZI MSHIRIKIANE KUWATUMIKIA WANANCHI WENU=KATIBU WA CCM MKOA WA PWANI

Katibu Wa CCM Mkoa wa Pwani Mhe. Bernard S. Ghaty akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha, Wajumbe wa Mabaraza, Jumuiya za Wazee, Viongozi wastaafu, makada wa CCM na wageni wengine wa waalikwa wakati wa ziara yake ya kutembelea Wilaya ya Kibaha Mjini akiambatana na Sekretarieti yake ya Mkoa ambayo ni Katibu wa Wazazi Mkoa, Elisante Msuya, Katibu Uenezi Mkoa David Mramba, Katibu wa UWT Fatma Ndee na Kaimu Katibu UVCCM Zainab Mketo

 

Na Zainab Nyamka, CCM Kibaha Mjini

Katibu Wa CCM Mkoa wa Pwani Mhe. Bernard Ghaty amewataka viongozi kuendelea kushirikiana na kuacha migogoro isiyokuwa na tija kwa sababu wote wanatumikia wananchi kwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Hayo ameyasema wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Kibaha Mjini akiambatana na Sekretarieti yake ya Mkoa ambayo ni Katibu wa Wazazi Mkoa, Elisante Msuya, Katibu Uenezi Mkoa David Mramba, Katibu wa UWT Fatma Ndee na Kaimu Katibu UVCCM Zainab Thabit wote kwa pamoja wamewataka wenyeviti wa matawi, mashina kutafuta wanachama wapya kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Ghaty amesema, hatataka kusikia tena viongozi wanaweka makundi, hata kama mwanachana anataka kukisaidia Chama basi ufuate utaratibu unaotakiwa na sio kuamua kwa utashi wake.

"Sitaki tena kusikia kuna migogoro kwa viongozi,  nyie wote ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi, leo hii mnaweka makundi huko wakati hata muda wenyewe haujafika wewe kama unataka kukisaidia Chama fuata utaratibu haujakatazwa ila kwa sasa tumuache Mbunge afanye kazi yake,"amesema Ghaty

"Wananchi wanapaswa kushirikiana na wale Viongozi waliopewa kusimamia Ilani, na kila kiongozi ajue wajibu wake, yawapasa kushirikiana kwa kiasi kikubwa," ameongeza.

Aidha, Katibu wa CCM Mkoa amewataka wenezi wa Chama katika kila Kata kuhakikisha bendera za CCM zinakua kila sehemu, na ziwe zimetapakaa kila kona ili viongozi wanapopita katika barabara hii waone Chama kipo.

Ghaty amesema, kama Muenezi wa Kata hana uwezo wa kununua bendera za Chama hata 5 basi hafai na hawana budi kumchagua tena ili awaongoze.

" Kama wewe ni kiongozi tena mwenezi wa Chama hauwezi kununua hata bendera, nawaagiza kuanzia sasa hivi hii barabara itapakae bendera ,hii ni barabara kubwa,viongozi wanapita ni lazima waone na wajue kuwa hapa Chama Cha Mapinduzi kipo na wanachama wapo wa kutosha, Kibaha mjini mnashindwa hata Kibaha Vijijini kila mahala pametapakaa Bendera ila na kwakuwa sasa hivi Ofisi yangu ipo hapa Kibaha basi nataka nihakikishe bendera zipo kila mahali,"amesema Ghaty

Ghaty amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha kwa kuendelea kuchagiza maendeleo ndani ya Jimbo la Kibaha Mjini na zaidi amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuunga mkono Serikali ya Rais mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye kuboresha miundo mbinu ya barabara, sekta ya afya na elimu kwa ujumla.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwl Mwajuma Amiri Nyamka amesema CCM Kibaha inampongeza Katibu wa CCM MKoa Bernard Ghaty kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano wa dhati.

Mwenyekiti CCM amesema, kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Ofisi ya Chama, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mbunge na hilo limechagiza maendeleo ndani ya Wilaya ya Kibaha.

Akitoa neno la shukrani kwa Katibu Wa CCM Mkoa, Mbunge wa Jimbo Silyvesrty Koka amesema Kwa asilimia kubwa Ilani ya CCM imetekelezwa kwa asilimia 95, upande wa miundo mbinu, katika sekta ya maji, elimu, , Umeme ,afya, barabara n.k.

"Tumetekeleza Ilani ya CCM kwa asilimia 95,tumeboresha upande wa elimu kwa kujenga Shule mpya na kuongeza madarasa katika shule zetu, katika sekta ya afya tumejenga Zahanati, tumejenga barabara  na tunaendelea kujenga ili kila eneo tuwe na barabara zenye kiwango cha lami," amesema

Ameongeza kuwa, " kwa upande wa maji wananchi wameanza kupata maji safi na salama na kuna mradi mpya wa ujenzi wa tanki la lita milioni sita (6,000,000) ambapo tayari mkataba umepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ukiwa bado kuidhinishwa ili tuanze kazi ya kuhakikisha Kibaha nzima inapata maji safi na salama na kuhusu umeme tuliomba Serikali itupunguzie bei za maunganisho sababu kuna maeneo Kibaha yapo kama Vijijini na tumekubaliwa,"

Katibu Wa CCM Mkoa wa Pwani Bernard Ghaty amefanya ziara hiyo ya kwanza toka kuteuliwa kwake akitokea Wilaya Kibaha Vijijini alipokua akitumikia Chama kwa nafasi ya Katibu wa CCM Wilaya.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya kibaha Mwl Mwajuma Amiri Nyamka akizungumza na kizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha, Wajumbe wa Mabaraza, Jumuiya za Wazee, Viongozi wastaafu, makada wa CCM na wageni wengine wa waalikwa na kuwataka waendelee kuhakikisha wanongeza wanachama na kuwasajili kwa mfumo wa kieletroniki. Kulia kwake ni Katibu Wa CCM Mkoa wa Pwani Mhe. Bernard S. Ghaty na  Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Mhe. Silyvesrty Koka. Walio meza ni kuu ni Katibu wa Wazazi Mkoa, Elisante Msuya, Katibu Uenezi Mkoa David Mramba, Katibu wa UWT Fatma Ndee na Kaimu Katibu UVCCM Zainab Thabit

Katibu Wa CCM Mkoa wa Pwani Mhe. Bernard S. Ghaty akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kibaha, Wajumbe wa Mabaraza, Jumuiya za Wazee, Viongozi wastaafu, makada wa CCM na wageni wengine wa waalikwa wakati wa ziara yake ya kutembelea Wilaya ya Kibaha Mjini akiambatana na Sekretarieti yake ya Mkoa ambayo ni Katibu wa Wazazi Mkoa, Elisante Msuya, Katibu Uenezi Mkoa David Mramba, Katibu wa UWT Fatma Ndee na Kaimu Katibu UVCCM Zainab Thabit




No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.