Habari za Punde

MWENYEKITI CCM KIBAHA MWAJUMA NYAMKA AKUTANA NA WAKUU WA SHULE NA KUSIKILIZA KERO ZAO

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mwl Mwajuma Amiri Nyamka akizungumza na wakuu wa shule (hawapo pichani) wakati wa  kikao kazi na  kusikiliza changamoto zao mbalimbali, Kikao hicho kilihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Siylvestry Koka na wajumbe wengine wa kamati ya Siasa Wilaya ya Kibaha.

Walimu wameaswa kuendelea kudumisha amani na utuvulivu katika jamii kwa sababu wao huanzia kutoa huduma ngazi ya kaya kupitia wanafunzi wao na mnaweza kupata uelewa wa kaya fulani kwa uharaka zaidi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mwl Mwajuma Amiri Nyamka wakati wa kikao kazi na Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mhe.Silyvestry Francis Koka, Mwenyekiti wa UWT Elina Mgonja, Mwenyekiti wa UVCCM Kibaha Mjini Ramadhan Kazembe, Mwenyekiti wa Halmashauri Mji Kibaha Mussa Ndomba pamoja na wajumbe wengine wa kamati ya Siasa.
Amesema, walimu wanasikilizwa katika jamii na wanaaminiwa kwa kila jambo pale wanapotoa ushauri au majadiliano na zaidi ni mshauri nasaha mkubwa wa mwanzo katika jamii na kutokana na hilo wasikubali kutumika na wanasiasa ambao wanatumia jukwaa la walimu kutaka kujitangaza.
"Msikubali kutumika na sisi wanasiasa, iwe ni wa CCM au Chama kingine kwa lengo la kuwavuruga, Kiongozi yoyote wa kisiasa anatakiwa afuate utaratibu pale anapohitaji kuja kwenu na hata nyie mnapomuhitaji kiongozi huyo yawapasa kufuata utaratibu,"amesema Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka.
"Kwa utaratibu ulio sahihi ni kuandika barua za maombi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya kwani yeye ndiyo kiunganishi baina yenu nyie walimu na sisi wanasiasa, na sio barua zenu kupitia kwa viongozi wa Chama,"amesema
Ameongeza kuwa, walimu mnatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi, viongozi mnaotakiwa kufanya nao kazi moja kwa moja ni wale ambao CCM imewakabidhi Ilani ya Uchaguzi ili waje kuitekeleza, kwa ngazi ya Taifa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, ngazi ya Jimbo ni Mbunge Mhe. Silyvestry Ftancis Koka, Madiwani wetu na kwenye ngazi ya Mtaa ni wenyeviti wa Serikali za Mtaa.
"Nawaomba muendelee kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi, na katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka ni 2024 nyie ndiyo nguzo kubwa ya kuweza kushika dola na hakuna chama kingine chochote kinachoweza kufanya haya yanayofanywa na Chama cha Mapinduzi,"amemalizia Mwl Mwajuma Nyamka
Kwa upande wa Mbunge Koka, akijibu maswali na maoni ya walimu amewahakikishia walimu kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania maslahi yao na kufikia tarehe 15/11/2023 suala la madeni sugu ya walimu liwe tayari limeangaliwa kwa namna gani linatatuliwa ikiwamo na kupata idadi kamili ya wanaodai.
Amesema, anafahamu changamoto wanazopitia walimu katika ufundishaji ila serikali ya Mama Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha maslahi ya walimu na kwa sasa wanafanya maboresho ya miundo mbinu kwa kujenga vyumba vya madarasa na kuna miradi ya Boost katika kila shule.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mhe.Silyvestry Francis Koka akizungumza na Wakuu wa Shule, akati wa  kikao kazi na kusikiliza hoja na changamoto zao mbalimbali.
 
Akijibu kuhusiana na lishe kwa watoto mashuleni, Mbunge Koka amesema suala hilo atalifikisha katika mikutano ya ndani ili kuweza kujadiliwa katika vikao vya kamati vya Chama na ikikubalika itapitishwa kwenye Ilani ya Chama kama ilivyo kwa sera ya elimu bure.
Aidha, Amewashukuru sana walimu kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kusimamia miradi ya shule pindi wanapokabidhiwa fedha na kuikamlisha ndani ya muda unaohitajika.
Walimu kwa pamoja wamemshukuru Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini Mwl Mwajuma Nyamka kwa kukutana nao na kusikiliza changamoto zao mbalimbali na pia wameomba vikao hivi viwe endelevu kwa sababu yeye Mwenyekiti ni Kiungo kikubwa baina yao na Serikali.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.