*RPC adai ni matatizo ya kawaida kukosea majina.......
Na Sufianimafoto Reporter, Mbeya
Barick Martin aliyedaiwa kuuawa na polisi katika jaribio la kupora fedha wafanyabiashara wa mbao katika Kijiji cha Nditu wilayani Rungwe ameibuka na kukana kuhusika katika tukio hilo na kuuawa kwa risasi.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mtanzania, Barick alisema kuwa baada ya taarifa kutangazwa kuwa ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi, baadhi ya ndugu kutoka Mikoa ya Arusha na Dar es Salaam , walipiga simu kijiji kwao Lufilyo wakiuliza kama ni kweli ameuawa.
Alisema waliwajulisha ndugu zake kuwa hajafariki, “taarifa hizo zilinistua sana , nikaenda Tukuyu Mjini nikanunua magazeti na kweli nikakuta nimetajwa kuwa moja ya watu waliouawa” alisema na kuongeza kuwa baadaye alikwenda polisi na kutoa taarifa kuwa yeye sio mtu aliyeuawa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema jina hilo lilitajwa kimakosa baada ya wananchi waliofika eneo la tukio hilo Juni 4, kuwatambua majambazi waliouawa na kumtaja Barick kuwa ndiye aliyeuawa wakati si yeye.
Alisema baada ya maiti kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, kusafishwa na ndugu wengine kufika, walimtambua mtu aliyetajwa kuwa ni Barick sio yeye na kwamba aliyeuawa alitambulika kwa jina la Bernad Anyosisye mkazi wa Nzovwe Mbeya.
Aidha Kamanda Nyombi alisema kukosea majina ni matatizo ambayo yanajitokeza na kwamba wananchi walikosea wakati wa kuwatambua majambazi waliouawa ambapo alisema tayari mwili wa Anyosisye umechukuliwa na ndugu zake kwa mazishi.
Hata hivyo Kamanda Nyombi alithibitisha kuwa taarifa za Barick kufungwa jela na kuachiwa April 26, mwaka huu ni za kweli na kwamba kilichokosewa ni taarifa kuwa ndiye aliyeuawa katika tukio la ujambazi katika kijiji Nditu wilayani Rungwe.
MUFTI MKUU TANZANIA KUJA NA ZIARA YA KUIMARISHA UONGOZI MKOA WA DODOMA
-
Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zubeir amesema Baraza limepanga kufanya ziara
rasmi mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kutembelea mikoa yote 26
nc...
2 hours ago
No comments:
Post a Comment