Habari za Punde

*SHIRIKA LA HANNS SEIDEL LATOA TUNZO NA VYETI KWA WAHITIMU WA MAFUNZO


Na, Ombeni Mhina, jijini Dar es Salaam

Washiriki wapatao 355 wamenufaika na mafunzo ya uongozi wa kisiasa kwa wanawake yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la kiserikali la Hanns Seidel Foundation hapa nchini tangu mwaka 2004 hadi sasa, hayo yamesemwa na Mary Tagalile Meneja wa Mradi wa shirika hilo hapa Tanzania wakati wa sherehe ya kutoa vyeti kwa washiriki wapatao 41 kutoka mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Iringa na Dodoma zilizofanyika katika Hotel ya Regency Park Mikocheni hapa Dar es salaam.
Shirika la Hanns Seidel Foundation ambalo linashirikiana na kituo cha Mafunzo na Utawala Bora katika kuandaa na kuendesha mafunzo hayo katika program maalum iliyoanzishwa hapa nchini mwaka 2004 ikiwa na lengo la kuwaendeleza wanawake katika swala zima la kujiamini wakati wa kugombea uongozi kwenye ngazi mbalimbali za uongozi.
Wanawake wapatao 150 kutoka vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini walinufaika na mafunzo hayo kati ya mwaka 2004 na 2005, wakati wanawake 105 wamenufaika na mafunzo kama hayo kwa nia ya kuibua chachu ya kujiamini kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini mwezi October mwaka huu.
Bi Tagalile alisema kuwa anaamini kupitia kauli mbiu ya shirika lake inayozingatia maneno makuu matatu, ambayo ni Demokrasia, Amani na Maendeleo kuwa, ili kuunda jamii huru kutoka kizazi kimoja hadi kingine, ni wajibu wa raia wote kushiriki kwa vitendo katika mchakato wa kuleta maendeleo ya Demokrasia, na kusisitiza kwamba Demokrasia ya kweli inahitaji utashi, elimu ya siasa na uraia ikilenga uelewa wa mtu binafsi, kwa kukuza vipaji walivyojaliwa ili vitumike katika kujenga mshikamano unaohitajika kijamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utawala Bora na Maendeleo ya Uchumi Profesa Maximilian Muya amewatata washiriki wa mafunzo hayo wawe chachu katika jamii na kupitia mafunzo waliyopata kupitia Taasisi yake ya Utawala Bora.
Washiriki wa mafunzo hayo, wamekiri kukumbana na changamoto mbalimbali kwenye maeneo watokayo, hata hivyo wameahidi kutumia mbinu walizojifunza pamoja na kubadilishana uzoefu walioupata kupitia mafunzo hayo.
Washiriki hao wamelishukuru Shirika la Hanns Seidel Foundation lenye makao makuu yake huko Munich nchini Ujerumani kwa kugharamia mafunzo yao, pamoja na Kituo cha Utawala Bora na Maendeleo ya Uchumi, kilichoandaa na kuendesha mafunzo ambayo yatawasaidia sana katika nyanja za maendeleo, kisiasa na kiuchumi huko waendako.


Mratibu wa Mafunzo wa Kituo cha Elimu cha Mafunzo ya Utawala bora, Betty Mkwawa (kushoto) akimkabidhi cheti, mhitimu wa mafunzo hayo, Grace Subwa, wakati wa sherehe za wahitimu hao zilizofanyika jijini Dar es Salaam juzi. Katikati ni Mkurugenzi wa Kituo hicho, Maxmillian Muya na Meneja wa Kampuni ya Hanns-Seidel Faundation, Marry Tagalile.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.