Habari za Punde

*RAIS JAKAYA APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO WA MABALOZI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi katika Ikulu ya Dar-Es-Salaam amepokea Hati za Utambulisho za Mabalozi kutoka Sweden na Norway na kufanya nao mazungumzo yanayohusu uhusiano na ushirikiano baina ya nchi zao na Tanzania.
Wote kwa nyakati tofauti wamempongeza Rais Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Wa kwanza kuwasilisha hati ni Balozi Lennarth Hjelmaker, wa Sweden ambapo Rais alianza mazungumzo kwa kutoa pole kwa nchi ya Sweden kwa kukumbwa na mashambulio ya mabomu ya kigaidi katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo wa Stockholm, Jumamosi iliyopita.

Uhusiano wa Tanzania na Sweden ni mkongwe ambapo Tanzania imekuwa ikipokea misaada ya maendeleo, mazingira na pia katika kusaidia jitihada mbalimbali za sekta binafsi.

Rais pia amepokea Hati za Utambulisho za Balozi Ingunn Klepsvik wa Norway.

Bibi Klepsvik ameanza mazungumzo yake kwa kumpongeza Rais Kikwete kwa Serikali ya Umoja iliyoundwa visiwani Zanzibar ambayo ni matokeo ya muafaka baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) na kisha kumpa salamu maalum na za binafsi kutoka kwa Waziri Mkuu wa Norway Mhe. Jens Stoltenberg.

“Nakupongeza sana kwa maridhiano na hali ya amani na utulivu wa visiwa vya Zanzibar, bila jitihada zako na kuyaunga mkono mazungumzo yale mafanikio yote haya yasingepatikana, hongera sana” Balozi Klepsvik amemwambia Rais.

“Rais Kikwete amemweleza Balozi kuwa hata yeye amefarijika sana na matokeo ya muafaka wa Zanzibar kwa sababu tangu kuingia madarakani aliweka azma ya kuanza mazungumzo na majadiliano ambayo yataleta maridhiano kwa manufaa ya visiwa vya Zanzibar, watu wake na Tanzania kwa ujumla” Rais amesema.

Wakati huohuo Rais amehuzunishwa na kutuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa mwanamuziki mkongwe Remmy Ongala aliyefariki usiku wa kuamkia leo hapa jijini.

“Tumepoteza mwanamuziki mkongwe na mbunifu, Remmy aliipenda na kuiheshimu kazi yake wakati wote, ni huzuni sana kwa wapenda muziki na hasa miziki ya kale” Rais amesema.

Rais Kikwete ni mpenzi wa Miziki yote ya kale na ya kisasa na hata alipokuwa amelazwa Muhimbili alifika hospitalini kumjulia hali yeye na mwanamuziki mwingine mkongwe Muhidin Gurumo, lakini akakuta Dr. Remmy amekwenda kufuatilia matibabu yake katika hospitali ingine ya jijini.

“Namwombea mapumziko mema na Mwenyezi Mungu amrehemu, tutamkumbuka sana” Rais amesema.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.