Na. Aron Msigwa –MAELEZO- Moroni, COMORO.
Vijana wanaomaliza masomo katika fani mbalimbali wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini jambo litakalopunguza idadi kubwa ya vijana wasio na kazi.
Akizungumza na wanafunzi na walimu wa kituo cha Mafunzo cha EMDAD cha mjini Moroni nchini Comoro, mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) mama Salma Kikwete ,alisema vijana wengi wanaomaliza masomo katika vyuo mbalimbali wanashindwa kujiajiri wenyewe wakati ujuzi wa kufanya kazi mbalimbali wanao.
Alisema hivi sasa nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya vijana ambao humaliza masomo katika fani mbalimbali ambao wanauwezo wa kujiajiri wenyewe lakini hawafanyi hivyo.
“Vijana wengi wanaomaliza masomo yao wengi husubiri kuajiriwa badala ya kujiajili wenyewe, natoa wito mnapomaliza masomo yenu mnakuwa tayari na ujuzi mjiajiri wenyewe na kuajiri wengine” alieleza.
Akiwa ameambatana na mwenyeji wake mke wa rais wa Comoro, mama Salma Kikwete alipata fursa ya kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na wanachuo na walimu wa chuo hicho huku akivutiwa na madarasa mawili moja likiwa la mafunzo ya kompyuta na lingine la ushonaji kwa vijana wa kike ambao hufundishwa kuajiajiri wenyewe pindi wanapomaliza masomo yao.
Kaimu mkuu wa chuo hicho Bw.Mohammed Jalal alimweleza mama Salma Kikwete kuwa mfumo wa elimu unaotolewa katika madarasa hayo unalenga kumjenga kijana uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira za serikali.
Alisema wanafunzi katika madarasa hayo hufundishwa kwa muda wa miezi sita na wanapomaliza hupatiwa vyeti vya ufaulu huku wale wanaoshindwa kufaulu kwa kiwango kilichowekwa hulazimika kurudia masomo yao.
Aliongeza kuwa wanachuo wanaofaulu vizuri zaidi ya kupewa vyeti hupewa mitaji ya fedha, vifaa au mikopo kwa ajili ya kuwawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za kuwapatia kipato.
“Mfumo wa elimu chuoni hapa unalenga kumjengea uwezo mwanachuo kuweza kujiajiri,kwa wale wanafaulu masomo yao vizuri hasa katika fani ya ushonaji tunawawezesha kwa vifaa vya kufanyia kazi na wakati mwingine tunawapatia mikopo ili waweze kuanzisha shughuli zao” alifafanua Bw. Jalal.
Pia akiwa chuoni hapo mama Salma Kikwete alipata fursa ya kutembelea karakana ya ufundi wa kutengeneza simu za mkononi ambapo aliweza kuona shughuli mbalimbali za masomo yaliyokuwa yakitolewa kwa wanachuo waliokuwepo.
Mwalimu wa darasa hilo Bw. Mohamed Reza alieleza kuwa vijana wengi wengi wanavutiwa na masomo yanayotolewa na karakana hiyo huku akibainisha kuwa mwamko wa kujifunza miongoni mwa vijana umekuwa mkubwa hali iliyopelekea wawe na muda tofauti wa vipindi vya masomo kutokana na uhaba wa madarasa.
“ Hivi sasa tuna vijana wengi wanakuja kuanza mafunzo, na hivi sasa tuna idadi ya vijana wapatao 100 katika karakana yetu ni ndogo, tumelazimika kuwa na madarasa 4 kwa muda tofauti ili kuwawezesha vijana wote kupata muda wa kujifunza” alibainisha Bw. Reza.
Kwa upande wake mke wa rais mama Salma Kikwete akihitimisha ziara yake chuoni hapo aliwapongeza wanachuo wote kwa kuamua kujifunza huku akiwataka kusoma kwa bidii ili pindi watakapomaliza masomo yao wajiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira za serikali ambazo ni chache.
No comments:
Post a Comment