Wanawake nchini Comoro wametakiwa kuungana na kutumia fursa na jumuiya mbalimbali walizo nazo ili kujiletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa leo na mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) mama Salma Kikwete alipotembelea kituo cha Mtandao wa Wanawake na Maendeleo mjini Moroni nchini Comoro ili kuona shughuli mbalimbali wanazofanya kufuatia mwaliko wa mke wa Rais wa nchini hiyo.
Amesema maendeleo ya wanawake mahali popote pale duniani yanatokana na juhudi zao wenyewe na kusisitiza kuwa umoja na upendo miongoni mwao na kufanya kazi kwa bidii huku wakithamini nafasi waliyonayo katika nchi yao ndiyo msingi wa maendeleo.
“ Ninajua na kuamini ni kuwa nguvu ya wanawake inatokana na wanawake kuungana na kuwa na upendo, kwa kufanya hivyo tutadhihirisha kuwa wanawake tuna nguvu kubwa sana, ni jeshi kubwa na wanawake tunaweza kuleta ukombozi katika familia na nchi zetu kwa ujumla” amesema.
Mama Salma Kikwete amewapongeza viongozi na wanachama wa mtandao wa wanawake nchini humo kutokana na malengo mazuri waliyojiwekea ili kuwakomboa wanawake licha ya kukabiriwa na changamoto mbalimbali huku akiwaomba kupanua huduma na mafunzo wanayotoa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ambayo hayajafikiwa.
“Nimeona mtandao wenu ni mkubwa na malengo yake ni mazuri ya kuwakomboa wanawake wa kada mbalimbali kutoka katika hali ya umasikini inayowakabili wanawake walio wengi, ninachofurahishwa sana na mtandao wenu ni malengo mazuri ya maendeleo mliojiwekea na nawaomba myatimize ” amesema.
Aidha amewakaribisha viongozi wa mtandao huo nchini Tanzania kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuona mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) .
“Nikiwa mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo nchini Tanzania nawakaribisha ili mje muone maendeleo makubwa yaliyofanywa na WAMA katika nyanja mbalimbali zikiwemo utoaji wa elimu kwa mtoto wa kike, mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi na suala zima la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi”
Awali akitoa maelezo kwa mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Salma Kikwete jinsi Mtandao wa wanawake na Maendeleo wa mjini, Moroni unavyofanya kazi mke wa Rais wa Comoro Bi.Ikililou Hadidja Aboubacar amesema kuwa mtandao huo unalenga zaidi kumkomboa mwanamke na kuimarisha mshikamano wa wanawake katika kutatua matatizo yao.
Ameongeza kuwa serikali kwa kutambua juhudi za wanawake wa Comoro imeweka kipaumbele kuhakikisha kuwa malengo ya mtandao wa wanawake na ustawi wao katika nchi ya Comoro unapewa kipaumbele.
“Mheshimiwa Rais wa Comoro pamoja na serikali anayoiongoza inatambua mchango wa wanawake katika kujiletea maendeleo na ndio maana mimi kama mke wa rais naungana nae na pia kuunga mkono juhudi za wanawake wa Comoro katika kujiletea maendeleleo licha ya changamoto mbalimbali zinazotukabiri” ameeleza Bi. Ikililou.
Naye mwenyekiti wa mtandao huo Bi.Jacqueline Assoumani katika risala yake aliyoitoa amemweleza mama Salma Kikwete kuwa mtandao wao ni taasisi isiyokuwa ya kiserikali ambayo inazishirikisha jumuiya takribani 100 na ulianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kumshirikisha mwanamke katika maendeleo ya nchi.
Amesema mtandao huo licha ya kuwashirikisha wanawake katika maendeleo ya nchi umelenga pia kumkomboa mwanamke kiuchumi,kupambana na ujinga, kuboresha afya ya akina mama na maisha ya wanawake hususani wanaoishi maeneo ya vijijini.
Ameongeza kuwa mtandao huo pia unajihusisha sana na maendeleo ya mtoto wa kike katika Nyanja ya elimu na afya hasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na kufafanua kuwa tayari mtandao huo mwaka 2006 ulianzisha mpango wa kupiga vita kutojua kusoma na kuandika kwa wanawake kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (kushoto) akipokea zawadi kutoka kwa Mke wa Rais wa Comoro Mama Hadidja Aboubacar Ikililoi Dhoinine wakati alipomtembelea nyumbani kwake mjini Comoro na kubadilishana mawazo. (juni 28.2011) Picha na Mwanakombo Jumaa- MAELEZO.
No comments:
Post a Comment