Habari za Punde

*CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO (TASWA) CHATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA MWANACHAMA WAKE RACHEL


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinaungana na familia na wanahabari wote nchini kuomboleza kifo cha Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Mtanzania Rachel Mwiligwa.

Rachel Mwiligwa, enzi za uhai wake.
TASWA imeshtushwa taarifa za kifo cha Rachel kilichotokea usiku wa kuamkia leo, hivyo tunatoa pole kwa familia yake, waandishi wa habari za michezo na wafanyakazi wenzake wote, wasanii na wanamichezo wengine katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mdau mkubwa wa michezo na burudani.


Kutokana na msiba huo, chama kinaandaa taratibu zake za kuwasilisha rambirambi kwa namna tulivyojiwekea, kwani marehemu hadi mauti yanamkuta alikuwa mwanachama mtiifu wa TASWA. Hivyo upo utaratibu kama mwenzetu akitangulia mbele ya haki namna gani tunatakiwa tufanye.

Lakini pia upo utaratibu mwingine nje ya chama ambao utahusu mtu binafsi kuwasilisha michango ya rambirambi, ambapo TASWA inawasiliana na wahariri wote wa habari za michezo wasaidie kukusanya michango ya rambirambi kwenye vyombo vyao, ambayo wataiwasilisha kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya kusimamia jambo hili.

Wajumbe hao ni Angela Msangi ambaye atakuwa Mratibu akisaidiwa na Mwani Nyangasa, ambao watashirikiana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, George John ambaye ni Katibu Msaidizi wa TASWA, Grace Hoka na Alfred Lucas ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Tunaomba ushirikiano wa wadau katika kufanikisha jambo hili.

Msiba kwa sasa kwa mujibu wa taarifa za awali upo Manzese Tiptop,tutaendelea kujulishana kadri zitakavyopatikana taarifa mpya.

Tunaomba waandishi wa habari za michezo, wasanii na wanamichezo kwa ujumla tumuenzi Rachel kwa masuala mbalimbali aliyokuwa akiyatilia mkazo ikiwemo kusimamia ukweli kwa kile alichokiamini na ndio maana tunasema tutaendelea kumkumbuka daima. 

Mungu amuweke mahali pema peponi. Amin

Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
11/05/2012        

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.