*KWA NINI LAMBALAMBA WANAPIGWA VITA DODOMA
*Kwanza ni lazima tufahamu Lambalamba
ni nini?
Hili ni kundi la watu ambalo
limeundwa kwa lengo la kujihusisha na vitendo vya kitapeli na ulaghai kwa
wananchi hususani wa vijijini, ili kujipatia mali zikiwemo fedha na mifugo ya
aina mbalimbali toka kwa wanavijiji katika mkoa wetu wa Dodoma.
Kundi hili ni mkusanyiko wa watu wa
jamii tofauti ambao wanatoka maeneo ya Rufiji , Pwani, Tanga na
Morogoro ambao wamekuja kuivamia jamii ya watu Dodoma ambayo nayo
ina mila na desturi zake katika mambo ya jadi.
Wamekuwa wakitumia mtindo wa
kujifanya kuwa wao ni waganga wa tiba za jadi kwamba wana uwezo wa kutoa vitu
vya kichawi katika majumba ya watu, sehemu za biashara
na pia kufichua wachawi, vitu ambavyo kwa hakika hawana
uwezo navyo.
Ili mtu akubalike kuwa ni mganga wa
tiba za jadi ni lazima afahamike katika eneo analofanyia shughuli zake hizo
kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi wa juu wa serikali na awe
na kibali cha kuendesha tiba hizo kisheria kitu ambacho kundi la lamba lamba
hawakidhi matakwa hayo.
Pia Mganga wa jadi kwa asili yake
hatakiwi kufanya kazi zake kwa kuita baadhi ya watu ni wachawi. Hutakiwa kutoa
tiba na kinga kwa kutumia miti shamba kulingana na uwezo wake, na sio
wanachofanya hao wanaojiita lambalamba hii ni tofauti na sheria
zinavyoelekeza.
Kwanza wanavijiji huchangishwa
na ndipo huitwa kundi hilo kuja kufanya kazi wanayodai ni ya
kufichua wachawi au washirikina, ambao wanadai wanavuta mali za watu wengine
kwao na kuwa matajiri.
Uchunguzi wetu umebaini kwamba
wanachofanya kundi la lambalamba kwa kushirikiana na washirika
wao, huwa wanapandikiza vitu kwenye nyumba, mashamba au sehemu za biashara za
mlengwa nyakati za usiku.
Baada ya kufanya hivyo ndipo
wanaondoka na kundi la watu na kwenda kutoa vitu ambavyo walishavipandikiza
kabla, kisha kinachotokea kwa anayefanyiwa hivyo ni kudhalilika yeye na familia
yake kuwa ni mchawi na kibaya zaidi hulazimishwa kutoa kiasi cha
fedha na mifugo kama adhabu na kutishiwa wasithubutu kwenda kutoa
taarifa Polisi.
Hili ni kosa la jinai na ukiukwaji
mkubwa wa haki za Binadamu, hatuwezi kuvumilia na kuwaacha wananchi wenzetu
kuendelea kupoteza fedha na mali zao kwa kuwanufaisha hao matapeli.
Zipo taarifa kuwa lambalamba hao
wanapofika vijijini hutafutiwa wanawake wa kuwapikia na kuwastarehesha. Huu ni
unyanyasaji wa kijinsia na jambo la hatari ambalo litachangia kuenea kwa
magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Haya yanayofanyika ni utapeli mkubwa
uliobuniwa na watu hao wa kujipatia fedha. Ni jambo linalodhalilisha,
linalojenga chuki, na uchochezi ndani ya jamii. Pia linahatarisha usalama
na amani pamoja na afya za wanawake na jamii kwa
ujumla.
Hili ni jambo la kukemea kuanzia
ngazi ya Familia, Kitongoji, Mtaa, Kata hadi Taifa. Wote kwa pamoja tunaona
athari zake tukemee kwa nguvu zote na wale wanaoendesha na kushabikia kundi hilo
watolewe taarifa ili wakamatwe.
Watu wasiogope kutoa ushahidi dhidi
ya kundi la lamba lamba na washirika wake hao wanaovuruga amani, utulivu,
usalama na kurudisha maendeleo nyuma.
Tupo kwenye karne ya Sayansi na
Teknolojia tusijiaibishe kwa kukumbatia mambo ya zama za kiza kwa kupumbazwa
akili zetu na matapeli waliobuni mradi wa kujipatia fedha na mali kwa ujanja wa
kupandikiza vitu kwenye nyumba, sehemu za biashara na mashamba, kisha baadaye
wanakuja kuvitoa na kudai wamefanya hivyo kwa uwezo wao wa kubaini wachawi na
kuifanya jamii yetu iishi kwa chuki na kukosa amani na kushindwa kufanya
shughuli za kujiletea maendeleo
Mwisho napenda kutoa wito kwa wananchi kwa
ujumla kupitia dhana ya
utii wa sheria kwa hiari kushirikiana kwa pamoja na Jeshi la
Polisi kwa kutoa taarifa za watu hao ili kuutokomeza uhalifu huu
ili jamii yetu iendelee kubaki salama na yenye amani na utulivu.
[D. A. MISIME – ACP]
KAMANDA WA POLISI [M] DODOMA
No comments:
Post a Comment