Habari za Punde

*TASWA FC, KIJITONYAMA VETERANS KUMENYANA KESHO UWANJA WA BORA

Na Mwandishi wetu, Dar
Timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa FC) kesho (Jumatatu) itacheza mechi maalum ya kirafiki dhidi ya timu ya Kijitonyama Veterans kwenye uwanja wa Bora, Kijitonyama.
Mechi hiyo imepangwa kuanza saa 10.00 jioni na imeandaliwa kwa lengo la kudumisha ushirikiano baina ya timu hizo mbili. Mwenyekiti wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa wachezaji wote watafungua swaumu zao mara baada ya mchezo huo.
Majuto ambaye pia ni kiongozi wa Kijitonyama Veterans alisema kuwa timu hizo mbili zinauhusiano mkubwa na kila mwaka huwa wanacheza mechi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na sasa imekuwa ni ‘mila’ yao.
Majuto alisema kuwa baadhi ya wachezaji wa Taswa FC pia ni wachezaji wa Kijitonyama Veterans kutokana na kukaa maeneo hayo.
“Taswa FC na Kijitonyama Veterans zinauhusiano wa karibu sana, baadhi ya wachezaji wa Taswa FC ni wachezaji wa Kijitonyama Veterans kutokana na kukaa maeneo hayo na kushughulika katika shughuli za kila siku za timu hiyo, naamini mechi hii ya ‘futari’ itakuwa nzuri, ushindano na wachezaji kukaa pamoja baada ya kuisha na ‘kufungua’ pamoja,” alisema Majuto.
Kuhusiana na Kijitonyama Veterans, Majuto alisema kuwa timu hiyo imejipanga vilivyo ili kuhakikisha inatoka na ushindi katika mechi hiyo. Alisema kuwa siku ya Jumatano, Kijitonyama itacheza mechi na timu ya Kijitonyama United na baada ya mchezo watafuturu pamoja.
“Mbali ya mechi ya Taswa FC, pia tutacheza na timu ya vijana wetu inayoshiriki ligi daraja la pili Kanda ya Dar es Salaam kwa lengo la kuwapongeza kufikia hatua hiyo,” alisema.
Alisema kuwa Kijitonyama Veterans itatumia mechi hiyo kuwapongeza wachezaji na makocha wao kwa lengo la kuwapongeza kufikia hatua hiyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.