Habari za Punde

*DAWASCO KUONGEZA UZALISHAJI KUTOKA LITA MILIONI 70 MPAKA 106 KWA SIKU.

Na Daudi Manongi-MAELEZO
Kaimu Meneja Uhusiano wa Shirika la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) Bi. Everlasting Lyaro amesema kuwa uzimaji wa mtambo wa Ruvu Juu kwa wakazi wa Dar es Salaam na Mji wa Kibaha mkoani Pwani  siku tatu kuanzia ijumaa ya tarehe 17 mpaka tarehe 19 Jumapili umelenga kuongeza uzalishaji kutoka lita milioni 70  mpaka lita milioni 106 kwa siku.
Bi Lyaro alisema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na Idara ya Habari Maelezo akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa za uzimaji wa mtambo wa Ruvu Juu.
Alisema kuwa sababu kubwa za kuzima mtambo huo ni kumruhusu mkandarasi (WABAG) kuunganisha mtambo mpya wa Maji na ule wa zamani ili kufanikisha kampeni ya kumtua mama wa Dar es Salaam ndoo kichwani kwa kumfikishia maji nyumbani kwake.
Kuzimwa kwa mtambo huo wa Ruvu Juu kutapelekea maeneo ya Mlandizi,Kibaha,Ubungo,Kimara,Kibamba,Kibangu,Makuburi,Tabata,Segerea na Kinyerezi kukosa maji kwa kipindi hicho cha masaa 72.

Aidha wananchi wa maeneo husika wanashauriwa kuhifadhi maji ya kutosha kwa siku hizo tatu na DAWASCO inaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kwani jitihada hizi ni maboresho ya kuwasogezea maji karibu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.