Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Hospitali ya Rufaa ya Amana Jijini Dar es Salaam imeboresha huduma za afya kwa kuweka mashine maalumu ya kutibu meno ijulikanayo kama (Ceramic dental machine) lengo ikiwa ni kuboresha huduma hizo katika hospitali za umma.
Akiongea katika mahojiano kwa njia ya simu Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Bw.Meshack Simwela ameeleza kuwa kwa sasa wataweza pia kutoa huduma ya afya kwa viongozi wa serikali pamoja na wabunge kupitia wodi maalum iliyotengwa kwa ajili yao ili kupata huduma hiyo wanapokuwa jijini hapa.
"Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutuletea mashine hii maalumu kwa ajili ya magonjwa yote ya meno na tunaishkuru pia kwa kutushauri kutenga wodi maalumu kwa ajili ya kuwatibia viongozi mbalimbali wakati wakiwa hapa Dar es Salaam,ushauri huo tumeupokea na tumeufanyia kazi", alisema Simwela.
Aliongeza kuwa maboresho hayo yatasaidia wananchi kupata huduma bora za afya na kupunguza gharama za matibabu na kuondoa usumbufu wa kwenda kutafuta huduma hiyo katika hospitali binafsi.
Bw. Simwela anabainisha kuwa mashine hiyo ilikuwa ikipatikana katika Hospitali chache za binafsi na matibabu yake huchukua muda mwingi na gharama kubwa jambo ambalo lilikuwa likiwaumiza wananchi wenye kipato cha chini, hivyo upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa msaada mkubwa sana.
Vilevile aliongeza kwa kutolea ufafanuzi suala la huduma ya wodi maalumu itakayokuwa ikitoa huduma za afya kwa viongozi na wabunge tayari imeshaanza kufanya kazi tangu mwezi Machi mwaka huu ikiwa na vyumba viwili vya wagonjwa mahututi (ICU) pamoja na vyumba 24 ambavyo vina sehemu ya kukaa, kulala pamoja na choo.
Aidha, amefafanua kuwa matibabu katika wodi hiyo yanaweza kulipiwa kwa bima ya afya au kwa fedha taslimu pia ameongeza kuwa wodi hizo hazijatengwa kwa ajili ya viongozi pekee bali zinaweza kutumika pia kwa wananchi wa kawaida watakaoweza kulipia gharama za matibabu zilizopangwa katika wodi hiyo.
Naye Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, David Langa amesema kuwa kufunguliwa kwa wodi hiyo kumesaidia sana waganga kuwepo katika vituo vyao vya kazi muda wote kwasababu huduma za afya kwenye wodi hiyo ni masaa 24 pia mganga anapomtibu mgonjwa anapatiwa asilimia 30 ya gharama za matibabu yale papo hapo,fedha hizo ni nje ya mshahara wa mwisho wa mwezi.
Ametoa rai kwa Serikali kuongeza mashine hizo maalumu kwa ajili ya magonjwa ya meno na kuziweka katika Hospitali mbalimbali ili kupunguza mlundikano wa wagonjwa wengi katika Hospitali moja.
No comments:
Post a Comment