Habari za Punde

*SERIKALI YASITISHA MASHINDANO YA UMITASHUMTA NA UMISSETA KUPISHA ZOEZI LA KUMALIZA UPUNGUFU WA MADAWATI NCHINI

Na Mwandishi Wetu, Dar
SERIKALI imetoa tamko la kuhairisha mashindano ya umoja wa michezo na Taaluma kwa shule za Msingi na Sekondari Tanzania (Umitashumta na Umisseta) ili kupisha zoezi la kumaliza upungufu wa madawati kwa shule za msingi na sekondari hadi hapo yatakapotangazwa tena.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Waziri wa ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene amesema mashindano hayo yameahirishwa ili kupisha zoezi la kumaliza upungufu wa madawati kwenye shule za msingi na sekondari kwani wadau muhimu wa mashindano hayo wote wanahitajika katika kumaliza tatizo hilo.

Amesema kuwa mpaka jana zilikuwa zimebaki siku 17 tu ambazo Rais John Magufuli alikuwa amezitoa kwa ajili ya kumaliza tatizo la upungufu wa madawati nchini hivyo amewataka wadau wote wa mashindano hayo kuvuta subira hadi hapo zoezi hilo litakapomalizika ndipo waendelee na mashindano hayo.

Amesema mashindano hayo yanashirikisha viongozi wote katika ngazi ya halmashauri, mikoa na wizara ambapo viongozi hao ndio wanaoshiriki katika kusimamia na kufanya ufutiliaji wa zoezi la utengenezaji wa madawati kama alivyoagiza Rais Magufuli.

“Kwa vile muda uliobaki kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la utengenezaji wa madawati ni finyu kwa maana siku 17 tu, serikali imeona ni busara sana kuahirisha michezo hiyo ili nguvu zote zielekezwe kwenye utengenezwaji wa madawati na michezo hiyo itafanyika tarehe nyingine itakayopangwa na kutangazwa,” amesema Simbachawene.

Ameongeza kuwa, “Nitoe wito kwa walimu wetu waendelee kuwahimiza wachezaji wote walioteuliwa kuendelea na mazoezi katika shule zao wanazosoma, hii itakuwa ni sehemu ya kujitayarisha kwa ajili ya mashindano hayo muhimu mara yatakapopangwa.”

Michezo ya Umisseta ilipangwa kufanyika kitaifa Jijini Mwanza ambapo ilitakiwa ianze June 13 hadi 22 mwaka huu huku ile ya Umitashumta ilipangwa kuanza June 25 hadi Julai 5 mwaka huu ikiwashirikisha jumla ya washiriki 6,200.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.