Habari za Punde

TAIFA STARS YALAZIMISHA SARE NYUMBANI KWA BENIN

TIMU ya Soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo imetoka sare ya bao 1-1 na Benin katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliochezwa katika dimba la Stade de I’Amitie mjini Cotonou, Benin.
Benin ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao kwa njia ya penati iliyopigwa na nahodha wao mkongwe Stephane Sessegnon, ambayo hata hivyo ilizua utata baada ya mpira kupigwa na mchezaji wa Benin na kumgonga mchezaji wao mkononi akiwa nje ya 18 ya Stars na mwamuzi kuamuru kupigwa penati langoni mwa Stars katika dakika ya 32.
Benin walionekana kuingia uwanjani na historia ya mwaka 2014 walipopiga mabao 4-1 katika uwanja wa Taifa huku wakionekana kucheza kwa kupania zaidi huku mwamuzi akionekana kutokuwa makini kuchezesha mchezo huo mara zote.
Kwani baada tu ya kutoa penati ambayo haikuwa ya haki kwa upande wa Stars dakika chache alifunika na kumnyima penati Simon Msuva wa Tanzania baada ya kusukumwa na beki wa Benin na kuangushwa ndani ya Penati boksi wakati akiwapita mabeki wawili na kuelekea kusawazisha.
Mwamuzi wa mchezo huo, Ligali Praphiou, alionekana kutokuwa makini kwa kutoa maamuzi yasiyo sahihi muda wote.
Maamuzi ya mwamuzi huyo yalionekana kuwapanikisha zaidi na kuwachanga wachezaji wa Taifa Stars lakini walitulizwa na beki wa kati Abdi Banda na Kipa Aishi Manula na kutulia kisha kujipanga na kucheza mpira na dakika ya 39 Simon Msuva alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 ambalo hata hivyo lilipanguliwa na kipa.
Kipindi cha pili Taifa Stars waliingia na kuonekana kucheza kwa kufuata maelekezo zaidi na kucheza pasi fupi ambazo zilisaidia kupata bao dakika ya 50 lililofungwa na Elias Maguli kwa kisigino akimalizia pasi ya Shiza Kichuya ambapo pia alikosa kufunga bao kama hilo alipochelewa kuunganisha pasi ya Simon Msuva iliyotokea upande wa kulia na mpira kumpita akiwa yeye na goli.
Kama vile kocha wa Taifa Stars alihitaji kufunga mabao zaidi alimtoa kiungo Rafael Daudi na kuingiza mshambuliaji Mbaraka Yusuf, Shiza Kichuya nafasi yake ikachukuliwa na Ibrahim Ajib, Hamis Abdallah akaingia Jonas Mkude baadae akaumia Mudathir akaingia Nurdin Chona.
Kwa matokeo hayo sasa huenda Tanzania ikapanda katika viwango vya FIFA ambayo hutolewa kila mwezi kwani Benin inashika nafasi ya 79 na Tanzania inashika nafasi ya 136 katika viwango vya Oktoba.
KIKOSI CHA TANZANIA: Aishi Manula, Himid Mao, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Hamisi Abdallah/Jonas Mkude dk 75, Simon Msuva/Boniphace Maganga dk 85, Mudathir Yahya/Nurdin Chona dk 92, Elias Maguli, Raphael Daudi/Mbaraka Yusuph dk 54 na Shizza Kichuya/Ibrahim Ajib dk 65
KIKOSI CHA BENIN: Fabien Farnole, Rodrigue Fassinou, Khaled Adenon, Cedric Hountonji, David Kiki, Djiman Koukou, Olivier Verdon, Jodel Dossou, Stephane Sessegnon, David Djigla Dossou na Steve Mounie.  

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.