Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa, akizungumza na waandishi wa habari
katika Banda la Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa kwenye Viwanja
vya Julius Nyerere Dar es Salaam, jana akitangaza kuhusu kufungwa kwa njia ya
Reli ya Kati kwa saa 72 ili kupisha ukarabati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka
ambapo njia hiyo itakuwa ikifungwa mara tatu kwa wiki kuanzia julai 13 mwaka
huu.
*************************
SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limetangaza kufunga njia ya Treni
ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Isaka Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga kwa
saa 72 kila wiki ambayo ni sawa na siku tatu kwa wiki ili kufanikisha ukarabati
wa reli hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Viwanja vya Maonesho
ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa, alisema kuwa ukarabati huo wa
takribani kilometa 970 unaotarajia kuanza Julai 13 mwaka huu utachukua miezi
mitatu zoezi ambalo kukamilika kwake kutaingiza faida
mara dufu ya usafiri huo na kwa Taifa.
“Waandishi wa Habari na Watanzania kwa ujumla, TRC sasa
tunakuja kuimarisha miundombinu ya Reli, tunafanya hivi kwa kuwa tunafahamu
mnahitaji huduma hizi, tunaomba mtuvumilie kwa siku ambazo tutafunga njia
hizi”alisema Kadogosa.
Aidha alisema kuwa ukarabati huo ni pamoja na kubadilisha Mataluma
na Reli kutoka ‘Pound 60 hadi Pound 80’ na kuunga maungio ya reli kwa umeme ‘Flash Butt Welding’ ili kupunguza wizi wa
vifungashio uliokuwa ukitokea siku za nyuma kwa kufungua bolt za viunganishio
vya reli ‘fish plate’ katika maungio ya reli.
Alizitaja faida za ukarabati huo kuwa ni pamoja na kuongezeka
kwa Speed ya Treni kutoka kilometa 35 kwa saa mpaka kilometa 75 kwa saa pamoja
na kuongeza uwezo wa ubebaji mizigo kwa Exeli moja kutoka Tani 13 hadi 18.
‘’Baada ya kukamilika ukarabati huu Treni zetu zitaweza kubeba
mizigo mingi zaidi kwa wakati mmoja, kwa haraka na usalama zaidi na pia
itapunguza ajali za mara kwa mara,
Lakini pia itaboresha mawasiliano na ishara za kuongezea Treni
kwa kuweka mfumo wa kisasa ujulikanao kama ‘Train Warranty System’ ili kuondoa
usumbufu wa mawasiliano kutoka kituo kimoja hadi kingine
Alibainisha kuwa ukarabati mwingine wa njia ya Reli kutoka
Tanga kwenda Arusha ulianza mapema mwaka
huu ambapo njia hiyo itaanza kutumika mwezi Desemba mwaka huu.
“Ndugu zangu wa mikoa ya Kaskazini mtaanza kunufaika na usafiri
wa treni ya Abiria kuanzia Desemba mwaka huu, yaani Sikukuu zaKrismas na Mwaka
mpya mtaenda nyumbani na Treni ya Abiria ya TRCälisema Kadogosa.
Akizungumzia ujenzi wa Reli ya Standard Gauge inayoendelea
kujengwa Nchini Kadogosa alisema kwa awamu ya kwanza kutoka Dar Es Salaam
kwenda Morogoro ujenzi huo umefikia asilimia 56.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja
Kadogosa, akisikiliza maelezo kutoka kwa fundi simu wa shirika hilo, John
Mandari, kuhusu simu zinazotumika kwa mawasiliano katika Stesheni za Treni
wakati alipotembelea katika Banda lao la Maonesho ya 43 ya Biashara ya
Kimataifa kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, leo.
No comments:
Post a Comment