Habari za Punde

SADC KUANZISHA MFUKO WA PAMOJA WA KILIMO NA CHAKULA

 MKURUGENZI wa Kilimo Chakula na Maliasili wa Nchi za SADC, Domingos Gowe, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, kuhusu mikakati mbalimbali ya kuimarisha miundombinu na ongezoeko la Chakula ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa pamoja wa kilimo kwa Kikanda kwa nchi za SADC. (Picha na Muhidin Sufiani)
Baadhi ya waandhi wa habari wanaoripoti mkutano wa SADC wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano na Mkurugenzi wa Kilimo Chakula na Maliasili wa Nchi za SADC, Domingos Gowe.
********************************
JUMUIYA ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imesema, ipo katika mkakati wa kuanzisha mfuko wa pamoja wa kilimo wa Kikanda kwa ajili ya kusaidia nchi wanachama wa jumuiya hiyo. 
 Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kilimo, Chakula na Maliasili wa SADC, Domingos Gove, alisema mfuko huo ni kwa ajili ya kusaidia changamoto zilizo katika sekta ya kilimo kwa wananchi walio ndani ya SADC.
“Tumetambua changamoto nyingi zilizo katika sekta ya kilimo ambazo  zinafanana kwa nchi zote ambazo zipo ndani ya jumiya hii, kwahiyo tutakachofanya ni kuhakikisha inapatikana kupitia mfuko huu , upatikanaji wa pembejeo ambazo hazitakwenda kuathiri mazingira kwa nchi husika pamoja na kuhamasisha ushindani na uzalishaji wa mazao bora"allisema.
Aidha alisema mfuko huo wa pamoja utasaidia katika matumizi bora ya teknolojia katika kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji, lengo likiwa ni kusaidia upatikanaji wa masoko pamoja na usalama wa chakula kwa nchi za SADC.
Gove alisema kupitia mkakati huo watahakikisha kunakuwa na miundombinu itakayofanikisha nchi wanachama kujikita kwenye kilimo kwa ajili ya kupata chakula cha kutosha kwa nchi zao.
"Kwenye mfuko huu ambao utaanzishwa kwa nchi za SADC utahakikisha kuna kuwa na usambazaji wa mbegu bora zisizo na magonjwa, upatikanaji wa soko kwa malighafi zinazohusika kwenye suala la kilimo,
Pia mkakati mwingine ni kuongeza ushindani na uzalishaji wa nafaka ili kuhakikisha kunakuwa na sera ya kulinda usalama wa chakula" alisema.
"Hii itasaidia pale nchi mojawapo itakapokuwa na tatizo la uhaba wa chakula tunasaidia kupeleka chakula kutoka kwenye nchi zenye chakula cha ziada,” alisema.
Aliendelea kusema vyakula ambavyo vitazalishwa vitazingatia suala la lishe, lengo ni kuhakikisha walaji wanakuwa na afya njema na imara kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo kwa nchi wanachama.
Wakati huohuo jumuiya hiyo imeeleza namna ambavyo imejipanga katika kuhakikisha nchi za SADC zinakuwa na miundombinu ya uhakika ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Habari, Matangazo na Machapisho ya Kamati Ndogo ya Kamati Kuu ya SADC Zamarad Kawawa, alieleza namna ambavyo Tanzania ilivyojiwekea malengo na mikakati katika ujenzi wa miundombinu.
“Tanzania tuko vizuri katika ujenzi wa miundombinu hasa bandarini, viwanja vyandege ,reli, na barabara kote kumeimarika kwa kiwango kikubwa,”alisema

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.